Trump anajiandaa kukutana na Kim Jong-un, huku Russia ikiikosoa Marekani
(last modified Sun, 23 Sep 2018 02:41:04 GMT )
Sep 23, 2018 02:41 UTC
  • Trump anajiandaa kukutana na Kim Jong-un, huku Russia ikiikosoa Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo amesema kuwa, Rais wa nchi hiyo Donald Trump anajiandaa kwa mkutano wa pili na Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini.

Pompeo amesema kuwa, kungali kuna mambo kadhaa yanayotakiwa kufanywa ili viongozi hao waweze kukutana kwa kikao chao cha pili. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema kuwa, mazungumzo yaliyofanyika wiki iliyopita kati ya Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un na Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini yanaweza kuwa ni hatua muhimu kwa ajili ya kuangamizwa silaha za nyuklia katika Peninsula ya Korea. Wakati huo huo, mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, viongozi wa Marekani wamekuwa wakibuni mzozo dhidi ya Korea Kaskazini kwa kutegemea ripoti za tume ya vikwazo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Vasily Nebenzya, mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa

Vasily Nebenzya ameyasema hayo akizungumza na Shirika la Habari la TASS la Russia sambamba na kukaribia mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, Wamarekani wamekuwa hawakubali uchunguzi ambao unaenda kinyume na malengo yao kuhusiana na Korea Kaskazini. Akiashiria kuwa Washington haitaki kuona mwelekeo wa mazungumzo kati yake na Korea Kaskazini unakuwa wa baina ya pande mbili, Nebenzya amesisitiza kwamba viongozi wa White House wanafanya juhudi kwa kutumia muundo wa vikwazo dhidi ya Pyongyang ili uwe wenye kudhamini malengo yake na muhimu zaidi ikiwa ni kuiadhibu nchi hiyo ya Asia kutokana na msimamo wake.

 

Tags