Mamia wapoteza maisha katika zilzala na tsunami nchini Indonesia
Mamia ya watu wamefariki dunia na wengine wengi kujeruhiwa kutokana na tsunami na mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokikumba kisiwa cha Sulawesi mashariki mwa kisiwa cha Borneo nchini Indonesia.
Zilzala hiyo yenye ukubwa wa 7.5 kwa kipimo cha rishta, imeutikisa mji wa Palu katika kisiwa hicho, na kusababisha vifo vya watu karibu 400 huku mamia ya wengine wakitoweka.
Sutopo Purwo Nugroho, msemaji wa Idara ya Kupambana na Majanga nchini humo BNPB amesema kuna uwezekano mkubwa idadi ya wahanga wa majanga hayo ya kimaumbile ikaongezeka kwani mamia ya watu hawajulikani waliko kufikia sasa.
Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Indonesia BMKG hapo juzi ilitoa tangazo kuhusu uwezekano wa kutokea tsunami nchini humo, lakini ikafuta tangazo hilo dakika 34 baadaye.
Mwezi uliopita wa Agosti, watu 319 walipoteza maisha kutokana na tetemeko jingine la ardhi katika eneo la Lombok nchini Indonesia.
Inafaa kukumbusha hapa kuwa, mwaka 2004 zilzala ya chini ya maji ilitokea katika Bahari Hindi na kusababisha tsunami katika nchi kadhaa huku Indonesia ikiathiriwa zaidi. Watu 170,000 walifariki dunia kwenye janga hilo la kimaumbile nchini Indonesia hususan katika mkoa wa Aceh.