Palestina yaishtaki Marekani ICJ kwa kuuhamishia ubalozi wake Quds
Palestina imewasilisha faili la malalamiko dhidi ya Marekani katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ), ikitaka kuangaliwa upya hatua ya Washington ya kuuhamishia ubalozi wake wa Israel katika mji mtukufu wa Quds, kutoka Tel Aviv.
Katika taarifa iliyotolewa jana Ijumaa, ICJ imethibitisha kwamba imepokea faili hilo la Palestina, inayotaka Marekani ishurutishwe kufunga ubalozi wake wa utawala wa Kizayuni wa Israel ulioko Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu.
Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema, Wapalestina kupitia Mamlaka ya Ndani ya nchi hiyi PA wametumia hoja kwamba, Hati ya Vienna ya Mwaka 1961 kuhusu Uhusiano wa Kidiplomasia imweka wazi kwamba, nchi ina haki ya kuweka ubalozi wake ndani ya mipaka ya nchi mwenyeji na kwa msingi huo, uwepo wa ubalozi wa Marekani mjini Quds ni kukanyaga haki ya kujitawala na mipaka ya Palestina.
Itakumbukwa kuwa tarehe 6 Disemba mwaka jana Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa Washington inaitambua Quds (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa Israel na kisha kuuhamishia ubalozi wake katika mji huo kutoka Tel Aviv.
Uamuzi huo umeendelea kupingwa na jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC.
Kadhalika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio likitangaza kuwa haliitambui Quds (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa Israel.