Wahajiri 466 waokolewa katika Bahari ya Mediterrania
Idara ya Mabaharia wa Uhispania imetangaza kuwa, wahajiri 466 waliokuwa mbioni kuvuka Bahari ya Mediterrania na kuingia barani Ulaya wameokolewa wakiwa ndani ya boti kumi hafifu katika maji ya Uhispania.
Taarifa ya idara hiyo imesema, wahajiri hao wameokolewa katika operesheni iliyofanyika siku ya Jumamosi na jana Jumapili, karibu na Lango Bahari la Gibraltar, mashariki mwa Uhispania, wakitokea kaskazini mwa Afrika.
Haya yanajiri wiki moja baada ya Jumuiya ya Misaada ya Uokoaji wa Baharini ya Hispania kufanikiwa kuokoa zaidi ya wahajiri 440 waliokuwa wanaelekea barani Ulaya kupitia safari hatarishi katika Bahari ya Mediterrania.
Katika hatua nyingine, shirika la habari la Anadolu linaloendeshwa na serikali ya Uturuki lilitangaza jana Jumapili kwamba, wahajiri watano wamekufa maji baada ya boti yao kuzama karibu na mji wa Enez mkoani Edirne, karibu na mji wa Alexandroupolis ulioko kaskazini mwa pwani ya Ugiriki.
Hata hivyo haijabainika idadi ya wahajiri waliokuwa kwenye boti hiyo iliyozama, lakini shughuli za kusaka miili zaidi zinaendelea.
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu zaidi ya wahajiri 300 waliokuwa mbioni kuelekea Uhispania pekee wamefariki dunia baada ya kuzama katika Bahari ya Mediterrania. Idadi ya wahajiri wote waliofariki dunia mwaka huu katika Bahari ya Mediterrania wakielekea Ulaya ni 1600.