Berlin yaitaka Russia izidishe uwekezaji nchini Ujerumani, yakaidi ushauri wa Trump
Waziri wa Uchumi na Nishati wa Ujerumani ameitolea wito Russia izidishe uwekezaji katika sekta ya uchumi nchini Ujerumani.
Peter Altmaier amesema leo pambizoni mwa mkutano wa Ujerumani na Russia mjini Moscow kuwa Berlin ingependelea kuona Russia ikizidisha uwekezaji wake katika sekta ya uchumi nchini Ujerumani. Altmaier ameongeza kuwa, Berlin inaiomba Moscow itoe kipaumbele zaidi kwa shughuli za biashara ndogondogo na za kati huko Ujerumani.
Hatua ya Waziri wa Uchumi na Nishati wa Ujerumani ya kukaribisha suala la kuimarishwa uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi yake na Russia imechukuliwa wakati Rais Donald Trump wa Marekani anaituhumu serikali ya Ujerumani kuwa ni mtegemezi aliyechupa mipaka wa gesi ya Russia.
Siku kadhaa zilizopita pia katika mazungumzo yake na Jens Stoltenberg Katibu Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato), Rais wa Marekani alieleza kuwa, nchi wanachama wa Nato zinaipatia Russia mabilioni ya dola kwa ajili ya kununua nishati na kwamba Berlin inanunua mafuta na nishati kutoka Moscow na kwa sababu hiyo Ujerumani ni mateka wa Russia.
Bi Angela Merkel Kansela wa Ujerumani amepinga tuhuma hizo za Trump kwamba Ujerumani imekuwa mateka wa Moscow na kusisitiza kuwa, Berlin inatekeleza siasa huru kwa mujibu wa maslahi yake na siasa zake za nje.