Seneti ya Marekani yataka kutouziwa silaha Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i49554-seneti_ya_marekani_yataka_kutouziwa_silaha_saudi_arabia
Kundi la Maseneta wa Marekani limewasilisha muswada unaotaka kupigwa marufuku uuzaji wa silaha za nchi hiyo kwa Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 16, 2018 14:46 UTC
  • Seneti ya Marekani yataka kutouziwa silaha Saudi Arabia

Kundi la Maseneta wa Marekani limewasilisha muswada unaotaka kupigwa marufuku uuzaji wa silaha za nchi hiyo kwa Saudi Arabia.

Maseneta waliowasilisha katika Bunge la Seneti jana Alkhamisi muswada huo unaojuikana kama "Sheria ya Mwaka 2018 ya Kuiwajibisha Saudi Arabia kwa Jinai za Yemen" ni pamoja na Bob Menende, Todd Young, Jack Reed, Lindsey Graham, Jeanne Shaheen, na Susan Collins.

Maseneta hao wamesema wamelazimika kuweka pembeni tofauti zao za kisiasa, na kuuwasilisha muswada huo kwa pamoja, ili kuhakikisha kuwa Saudia inabebeshwa dhima ya mauaji yanayoendelea nchini Yemen, na pia mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari mkosoaji wa utawala wa Riyadh, Jamal Khashoggi.

Seneta Jack Reed ambaye ni mwanachama wa Kamati ya Silaha ya Bunge la Seneti la Marekani amesema ingawaje wanapongeza hatua ya Washington ya kuwawekea vikwazo watu 17 wanaohusishwa na mauaji ya Khashoggi, lakini hatua kali zaidi zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya Saudia.

Bunge la Seneti ya Marekani

Mwezi uliopita, Rais Donald Trump alisema licha ya Washington kukabiliwa na mashinikizo ya kuangalia upya uhusiano wake na Riyadh kufuatia mauaji ya Khashoggi, lakini Marekani itakuwa inajiadhibu yenye iwapo itaamua kusimamisha uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia. Alisema, "Iwapo hawatanunua silaha kutoka kwetu, basi watanunua kutoka Russia na China, tutakuwa wapumbavu sana iwapo tutapoteza dola bilioni 110, na badala yake nchi nyingine zistafidi nazo."

Kwa mujibu wa uchunguzi wa taasisi ya Stockholm International Peace Research Institute (SIPRI), Saudi Arabia inashika nafasi ya kwanza kwa kununua silaha katika eneo la Mashariki ya Kati huku Marekani ikiwa muuzaji mkubwa zaidi wa silaha duniani.