Marekani yaendelea kuisakama Korea Kaskazini, yamuwekea vikwazo anayeisaidia kununua mafuta
(last modified Tue, 20 Nov 2018 15:17:00 GMT )
Nov 20, 2018 15:17 UTC
  • Marekani yaendelea kuisakama Korea Kaskazini, yamuwekea vikwazo anayeisaidia kununua mafuta

Katika mwendelezo wa vikwazo vya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini, Wizara ya Fedha ya nchi hiyo imemuwekea vikwazo mfanyabiashara mmoja wa Russia kwa tuhuma za kuidhaminia mafuta Pyongyang.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha ya Marekani imesema kuwa, kwa mujibu wa amri ya utekelezaji nambari 13722, imeamua kuliweka katika orodha ya vikwazo jina la Vladlen Amtchentsev, raia wa Afrika Kusini mzaliwa wa Russia, kutokana na kuwa na uhusiano na Korea Kaskazini. Imeongeza kwamba, Amtchentsev amewekwa katika orodha ya vikwazo ya Marekani kutokana na yeye kushirikiana na Shirika la Velmur Management Pte. Ltd katika kuifikishia mafuta Korea Kaskazini. Mwezi Oktoba mwaka jana, ofisi ya kudhibiti fedha za kigeni nchini Marekani ililiweka shirika hilo katika orodha ya vikwazo kutokana na kujishughulisha na sekta ya viwanda ya Korea Kaskazini.

Licha ya Trump kukutana na Kim Jong-un na kutiliana saini, lakini bado nchi yake inaifanyia miamala mibaya Pyongyang

Kuendelea vikwazo vya Marekani dhidi ya serikali ya Pyongyang kunajiri katika hali ambayo nchi hiyo imepiga hatua kubwa kwa ajili ya kupatikana amani katika eneo la Peninsula ya Korea ikiwemo kubomoa eneo la kufanyia majaribio ya silaha zake za nyuklia, huku kwa upande wake Marekani ikiwa bado haijatekeleza hatua yoyote ya kivitendo kwa ajili ya kutekeleza ahadi zake kupitia fremu ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande mbili tarehe 12 Juni mwaka huu nchini Singapore. Korea Kaskazini imeeleza bayana kwamba, Washington haina nia ya kweli ya kutekeleza makubaliano ambayo yalifikiwa baada ya kukutana viongozi wa nchi hizo mbili.

Tags