Eritrea, Misri na Saudia zaongoza kwa kuwafunga jela waandishi wa habari
Ripoti mpya ya Kamati ya Kuwalinda Wanahabari CPJ imesema Eritrea ndiyo nchi yenye idadi kubwa ya waandishi wa habari waliofungwa jela katika eneo la Chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika.
Ripoti hiyo imesema waandishi wa habari wapatao 16 wapo kizuizini katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, ikifuatiwa na Cameroon inayowazuilia wanahabari saba.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Kamati ya Kuwalinda Wanahabari, wanahabari 30 wamefungwa jela katika nchi tano za eneo la Chini ya Jangwa la Sahara kufikia Disemba Mosi mwaka huu, ambapo mbali na Eritrea, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Somalia zinaongoza katika orodha hiyo.
Kimataifa, wanahabari 251 wamekamatwa na kufungwa jela kufikia Disemba Mosi mwaka huu, huku China, Misri na Saudi Arabia zikiwafunga jela waandishi wa habari wengi mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana.
Miongoni mwa waandishi wa habari 47 ambao wapo kizuizini nchini China, 10 wanatoka katika jamii ya Waislamu wa Uighur wanaokandamizwa, katika eneo la Xinjiang wakiwa wamefungwa jela bila hata kufunguliwa mashitaka.
Mwezi uliopita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema jumla ya waandishi wa habari 85 na wafanyakazi wengine katika sekta ya upashaji habari wameuawa tokea mwanzoni mwa mwaka huu 2018 katika sehemu mbalimbali duniani.