Ripoti: Wanahabari 80 wameuawa mwaka huu 2018
Jumuiya ya Maripota Wasio na Mipaka (RSF) imesema waandishi wa habari na wafanyakazi wengine katika sekta ya upashaji habari 80 wameuawa mwaka huu 2018 katika sehemu mbalimbali duniani.
Katika ripoti yake ya kila mwaka, shirika hilo lenye makao yake nchini Ufaransa limesema matamshi ya chuki yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa yamechangia katika ongezeko la mauaji dhidi ya wanahabari duniani.
Ripoti ya Shirika la Maripota Wasio na Mpaka imeashiria mauaji ya Jamal Khashoggi, mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal Saud, ambaye aliuliwa na mwili wake kukatwa vipande vipande, alipoingia kwenye jengo la ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki mnamo tarehe Pili Oktoba mwaka huu na kusema kuwa, chuki za wazi za baadhi ya wanasiasa, viongozi wa kidini na wafanyabiashara wakubwa dhidi wanahabari zimechangia kushuhudiwa ongezeko la mauaji ya waandishi wa habari mwaka huu, ikilinganishwa na mwaka jana.
Ripoti ya mwaka jana 2017 ya RSF ilisema wanahabari 65 waliuawa mwaka huo katika sehemu mbalimbali duniani.
Jumuiya hiyo imesema waandishi habari katika baadhi ya nchi duniani zikiongozwa na Saudi Arabia na Misri, hawana uhuru wa kujieleza na wanafanya kazi katika mazingira ya mashinikizo na ukandamizaji.
Jumuiya ya Maripota Wasio na Mipaka imeongeza kuwa, waandishi wa habari wapatao 348 wanazuiliwa katika sehemu mbalimbali duniani, huku wengine 60 wakishikwa mateka.