Onyo la Russia kuhusu kuingilia kijeshi Marekani mgogoro wa Venezuela
(last modified Wed, 30 Jan 2019 12:54:12 GMT )
Jan 30, 2019 12:54 UTC
  • Onyo la Russia kuhusu kuingilia kijeshi Marekani mgogoro wa Venezuela

Matukio ya kisiasa yaliyojiri karibuni katika nchi yenye utajiri mkubwa wa mafuta ya Venezuela na makabiliano yanayozidi kupamba moto baina ya wapinzani na serikali ya mrengo wa kushoto ya nchi hiyo yameingia kwenye awamu nyeti na hasasi.

Jumatano iliyopita, kiongozi wa upinzani Juan Guaido, akiungwa mkono waziwazi na Marekani na waitifaki wake, alijitangaza rais wa muda wa Venezuela, hatua ambayo serikali na wananchi wa nchi hiyo wameitaja kuwa ni mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Nicolas Maduro, rais halali aliyechaguliwa na wananchi.

Kulia ni Rais halali wa Venezuela Nicolas Maduro; na kushoto ni mpinzani wa serikali Juan Guaido aliyejitangaza rais mwenyewe

Hivi sasa Marekani na waitifaki wake wanaendelea kumuunga mkono Guaido wakiwa na lengo la kuipindua serikali ya Venezuela. Mansour Moozami, mtaalamu wa masuala ya Amerika ya Latini analizungumzia suala hilo kwa kusema: Kwa kumuunga mkono mtu aliyejitangaza na kujiita rais wa muda wa Venezuela, Marekani, waitifaki wake wa Ulaya na baadhi ya nchi za Amerika ya Latini, zimeanzisha mtindo hatari sana, ambapo kama jamii ya kimataifa haitachukua hatua mwafaka kukabiliana nao, mtindo huo hatari unaweza kuenea katika nchi zingine pia na kusababisha madhara makubwa kwa mhimili wa demokrasia. 

Suala hilo limekabiliwa na jibu na radiamali kali ya Russia, ambayo ni muungaji mkono wa rais halali wa Venezuela, Nicolas Maduro. Jana usiku, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Ryabkov alizitaka nchi za Magharibi ziachane na mpango, fikra au dhana yoyote ya kutaka kujiingiza kijeshi nchini Venezuela.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Ryabkov

Jibu na radiamali ya Russia kuhusu uwezekano wa Marekani kuingilia kijeshi mgogoro wa Venezuela imetokana na ushahidi unaotilia nguvu suala hilo. Tetesi  na uwezekano wa Marekani kutumia jeshi lake kwa ajili ya kuiangusha serikali ya Venezuela ulipata nguvu zaidi katika kikao na waandishi wa habari kilichofanywa juzi Jumatatu na John Bolton, mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani ili kutangaza vikwazo vipya vya kiuchumi dhidi ya Caracas. Katika kikao hicho, Bolton alitangaza vikwazo dhidi ya shirika la mafuta na gesi la Venezuela na akasisitiza pia kwamba, kama alivyotangaza rais wa Marekani, Donald Trump, machaguo yote kuhusiana na Venezuela yako mezani.

Lakini saa moja tu baada ya kikao hicho, ilisambazwa picha ya Bolton alipokuwa kwenye kikao hicho, akiwa ameshika karatasi kadhaa. Kwenye moja ya karatasi hizo yaliandikwa maneno "(Kutuma) askari 5,000 Colombia". Kuchapishwa kwa picha hiyo kulipelekea kuenea uvumi kwenye mitandao ya kijamii kwamba karibuni hivi, huenda Marekani ikatuma askari wake nchini Colombia, ambayo ina mpaka wa pamoja na Venezuela.

Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, John Bolton

Japokuwa serikali ya Colombia imetangaza kumuunga mkono Juan Guiado, lakini imekanusha habari za uwezekano wa kutumwa askari wa Marekani nchini humo kwa ajili ya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Venezuela.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi za bara la Amerika, nchi yoyote ile kati ya hizo, haitakiwi kutuma askari wake kwenye nchi nyingine ya bara hilo. Endapo Marekani itatuma wanajeshi wake huko Colombia itakuwa imeyakiuka makubaliano hayo.

Pamoja na hayo, uwezekano wa Marekani kuingilia kijeshi nchini Venezuela kwa madhumuni ya kumwondoa madarakani kwa nguvu rais Maduro, umepata nguvu zaidi wakati huu kuliko wakati wowote ule tangu ulipoanza mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.

Ni wazi kwamba suala hilo limeitia wasiwasi mkubwa Russia. Kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Facebook, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo Maria Zakharova, ameitahadharisha Marekani na kuchukua hatua yoyote itakayovuruga uthabiti katika eneo la Amerika ya Latini hususan nchini Venezuela.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova

Huku akiukosoa uingiliaji wa wazi na usio na sababu wa Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela, Zakharova ameandika: Kama ilivyo kawaida yao ya kila mara, Wamarekani wanakwepa kutoa jibu rasmi kwa masuala kama haya, lakini inapasa watoe jibu kuhusu maandiko ya mkono ya kichochezi ya Bolton; na Russia inangojea maelezo ya Washington.

Kwa mtazamo wa Russia, katika kutekeleza sera zake za kihasama na za uingiliaji wa masuala ya Amerika ya Latini, serikali ya Trump inataka kuchukua hatua zitakazoidhoofisha na hatimaye kuiangusha serikali ya mrengo wa kushoto ya Venezuela na kuiweka madarakani serikali kibaraka ya mrengo wa kulia katika nchi hiyo ya Amerika ya Kusini.

Muelekeo huo wa Marekani unapingana waziwazi na sheria za kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov alisema jana kuwa: Marekani imekiuka sheria za kimataifa kuhusiana na Venezuela.

Inavyoonekana, ili kukabiliana na sera za utumiaji mabavu na za uchukuaji hatua za upande mmoja za Marekani, sambamba na kulinda maslahi yake ya kistratejia nchini Venezuela, Russia imekusudia kuchukua hatua za dharura kwa ajili ya kumhami na kumuunga mkono Nicolas Maduro, rais halali wa nchi hiyo.../ 

Tags