Safari ya Mohammad Bin Salman nchini Malaysia na Indonesia yaahirishwa ghafla
(last modified Sun, 17 Feb 2019 05:04:00 GMT )
Feb 17, 2019 05:04 UTC
  • Safari ya Mohammad Bin Salman nchini Malaysia na Indonesia yaahirishwa ghafla

Safari ya Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia nchini Malaysia na Indonesia imearishwa ghfla bila kutolewa sababu.

Shirika Rasmi la Habari la Malaysia 'Bernama' lilimnukuu Mahathir Bin Mohamad, Waziri Mkuu wa Malaysia Jumamosi ya jana akiongea na waandishi wa habari kwamba, mwanamfalme huyo wa Saudia amevunja ghafla safari yake nchini humo. Kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Malaysia, Bin Salman amevunja safari hiyo bila kutoa sababu yoyote na kwamba safari hiyo itafanywa wakati mwingine ambao haujawekwa wazi. Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia pia imetangaza habari ya kuvunjwa safari ya Mohammad Bin Salman nchini humo na kuongeza kwamba, bado hakujatajwa tarehe nyingine mpya ambayo mwanamfalme huyo atakapoitembelea nchi hiyo.

Maandamano makubwa ya Wapakistan wakipinga Bin Salman kukanyaga ardhi yao

Uamuzi wa kuahirishwa safari hiyo ndani ya nchi hizo umechukuliwa masaa machache baada ya jamii na asasi mbalimbali ndani ya mataifa hayo kutangaza kwamba zitafanya maandamano makubwa katika miji ya Kuala Lumpur na Putrajaya ya Malaysia na pia mji wa Jakarta, Indonesia kulaani jinai na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu unaofanywa na Mohammad Bin Salman, kuanzia ukandamizaji dhidi ya maulama na wanaharakati wa Saudia wanaoshikiliwa jela, mauaji na jinai kubwa dhidi ya raia wa Yemen, jinai ya kutisha dhidi ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari mkosoaji wa Saudia aliyeuawa katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki na uhusiano mkubwa alionao na utawala haramu wa Israel. Hii ni katika hali ambayo Jumamosi ya jana pia Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ilitangaza habari ya kuahirishwa safari ya mwanamfalme huyo wa Saudia nchini humo kwa muda wa siku moja.