IAEA yathibitisha tena Iran inafungamana na mapatano ya nyuklia
Wakala wa Kimataifa wa Nishati Atomiki, IAEA kwa mara ya 14 sasa umethibitisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafungamana kikamilifu na mapatano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekeezaji, JCPOA, yaliyofikiwa baina ya Iran na madola sita makubwa duniani 2015.
Katika ripoti yake ya kila miezi mitatu iliyotangazwa Ijumaa, IAEA imesema Iran imefungamana na masharti yote ya urutubishaji urani ambayo yamewekwa katika mapatano ya JCPOA. IAEA pia imesema imweza kutekeleza ukaguzi katika vituo vya nyuklia vya Iran bila vizingiti vyovyote.
Naye Balozi wa Iran katika taasisi za kimataifa mjini Vienna, makao makuu ya IAEA Kazem Gharibabadi amethibitisha ripoti ya wakala huo wa Umoja wa Mataifa wa nishati ya atomiki ambayo imebaini wazi kuwa Iran inafungamana na mapatano ya nyuklia ambayo yalianza kutekelezwa Januari 2016.
Gharibabadi amesema pamoja na kuwepo jitihada kubwa za baadhi ya maadui na wanaoitakia Iran mabaya ambao walilenga kupotosha muelekeo wa IAEA na jamii ya kimataifa, lakini Iran inaendelea na uhusiano wake mzuri na wakala huo wa Umoja wa Mataifa wa nishati ya atomiki.
Hali kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran mjini Vienna amesisitiza kuhusu ulazima wa IAEA kuendelea na kazi zake za kitaalamu pasina kupendelea upande wowote. Aidha amekosoa baadhi ya wale ambao wanaiwekea IAEA mashinikizo ya kisiasa.
Gharibabadi amesema Iran imekuwa ikiwajibika kikamilifu kuhusu ahadi zake katika JCPOA na kuongeza kuwa, wanachama waliosalia katika JCPOA lazima wahakikishe kuwa Iran inafaidika kwa kusalia katika mapatano hayo.
Mapatano ya IAEA yalifikiwa kwa mara ya kwanza Julai 2015 baina ya Iran na wawakilishi wa nchi za kundi la 5+1 ambazo ni China, Ufaransa, Marekani, Russia, Uingereza na Ujerumani pamoja na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya. IAEA imekuwa ikichunguza na kusimamia shughuli zote za nyuklia za Iran.
Mnamo Mei 2018, Marekani ilichukua uamuzi wa upande moja wa kujiondoa katika mapatano ya JCPOA, hatua ambayo imelaaniwa vikali kimataifa na kupelekea watawala wa Washington kuzidi kutengwa.