Maduro: Wananchi wa Venezuela watasimama imara kupambana na madola ya kibeberu
(last modified Sat, 23 Feb 2019 16:31:20 GMT )
Feb 23, 2019 16:31 UTC
  • Maduro: Wananchi wa Venezuela watasimama imara kupambana na madola ya kibeberu

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema kuwa serikali ya Caracas kwa ushirikiano na wananchi wa nchi hiyo watasimama kidete kupambana na madola ya kibeberu na hawatorudi nyuma katika suala hilo.

Rais Maduro amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na televisheni ya Hispan TV na kuongeza kuwa, Venezuela ina nguvu kubwa za kusimama imara kupambana na madola ya kibeberu duniani na kuleta kigezo bora cha kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

Amezungumzia pia vitisho vilivyotolewa na rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu kuivamia kijeshi Venezuela na kusema kuwa uchunguzi wote wa maoni unaonesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Venezuela wanapinga uingiliaji au vitisho vya kijeshi dhidi ya nchi yao. Amesema, wananchi wote wa Venezuela wana msimamo mmoja kuhusiana na vitisho hivyo vya Trump.

Waungaji mkono wa Maduro nchini Venezuela

Tayari Venezuela imeshafunga mipaka yake na Columbia na Brazil ili kuzuia njama za Marekani za kuingiza silaha nchini humo kwa jina la misaada ya kibinadamu.

Rais wa Venezuela vile vile amesema, lengo kuu la Trump ni kutaka kuipigisha magoti nchi hiyo na kuongeza kuwa, rais wa Marekani ana misimamo ya kuchupa mipaka, isiyo na kimantiki na isiyokubalika kabisa kuhusiana na Venezuela.

Amma kuhusina na uungaji mkono wa kidiplomasia na kisiasa wa Iran kwa Venezuela na wananchi wake, Rais Maduro amesema, Caracas muda wote imekuwa ikipata uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Vile vile amesema: Ninamshukuru sana Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na ninamuhesabu kuwa ni mwenye shakhsia ya kupigiwa mfano kama ambavyo ninamshukuru pia Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags