Bemba ataka ICC impe fidia kwa kumfunga miaka 10 bila hatia
Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jean-Pierre Bemba, ambaye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC mwaka jana ilimuondoa hatiani, anaitaka mahakama hiyo ya mjini The Hague nchini Uholanzi impe fidia ya Yuro milioni 68 kwa kutompata na hatia katika kesi ya jinai za kivita iliyokuwa ikimuandama.
Kupita wakili wake, Peter Haynes, Bemba amesema jumba lake la kifahari nchini Ureno na ndege saba zimeharibika kutokana na yeye kuwekwa kizuizini kwa muda wa muongo mmoja ilihali hakuwa na hatia.
Wakili huyo amesema kwa msingi huo wameanzisha mchakato wa kuitaka ICC impe Bemba fidia ya Yuro milion 68 sawa na Dola 76.5 za Marekani. Anasisitiza kwamba iwapo atapewa pesa hizo, yuko tayari kutoa Yuro milioni 22 kwa ajili ya watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Bemba, mwenye umri wa miaka 55, ambaye amekuwa katika kizuizi cha ICC tokea mwaka 2008 alipatikana na hatia ya kuhusika na jinai dhidi ya binadamu na kuhukumiwa kifungo cha miaka 18 gerezani mwaka 2016.
Hata hivyo Juni mwaka jana, ICC ilimuachia huru kwa muda na kwa masharti maalumu. Majaji wa rufaa walisema Bemba hawezi kubebeshwa lawama ya mauaji na ubakaji wa raia uliofanywa na wanajeshi waliokuwa chini ya amri yake.
Bemba ambaye alikuwa makamu wa rais katika serikali ya mpito ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya Julai 2003 na Disemba 2006, alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2006 ambapo Joseph Kabila aliibuka mshindi.