Wanadiplomasia 50 wa Marekani wamtaka Trump ajiunge tena na JCPOA
Wanadiplomasia 50 wa zamani wa Marekani wamemwandikia barua Rais Donald Trump wa nchi hiyo wakitaka kurejea Washington katika makubaliano ya nyuklia baina ya nchi za kundi 5+1 na Iran maarufu kwa kifupi kama JCPOA.
Wanadiplomasia na majenerali 50 wastaafu wa Marekani pia wamemtaka Trump afute vikwazo vya upande mmoja vya serikali ya Washington dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Wakieleza sababu za udharura wa Marekani kujerea katika makubaliano hayo, majenerali na wanadiplomasia hao wastaafu wa Marekani wameashiria ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) iliyothibitisha tena kwamba Iran imeendelea kuheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA licha ya Marekani kujiondoa katika makubaliano hayo na kurejesha tena vikwazo dhidi ya Tehran na kusema: Hatua hiyo ya Iran ya kuendelea kutekeleza makubaliano ya kimataifa ni kielelezo kwamba, Tehran inaheshimu majukumu yake.
Ijumaa ya tarehe 22 Februari Wakala wa kimataifa wa Nishati ya Atomiki ulitoa taarifa na kuthibitisha kwa mara ya 14 kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeheshimu na kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Makundi 51 yanayotetea demokrasia nchini Marekani pia siku chache zilizopita yalitoa taarifa ya pamoja yakiwataka wabunge wa nchi hiyo kufanya jitihada za kuirejesha Marekani kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Trump alichukua hatua ya upande mmoja ya kuiondoa nchi yake katika mapatano ya JCPOA hapo tarehe nane Mei mwaka jana na kisha akarejesha vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hatua hiyo ya Trump na ambayo ilitokana na kuchochewa na lobi ya Kizayuni hadi hivi sasa inaendelea kulaaniwa vikali ndani na nje ya Marekani.