Russia yaionya Marekani isijaribu kuyawekea vikwazo mashirika yake nchini Venezuela
(last modified Thu, 14 Mar 2019 02:30:46 GMT )
Mar 14, 2019 02:30 UTC
  • Russia yaionya Marekani isijaribu kuyawekea vikwazo mashirika yake nchini Venezuela

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetoa onyo kwa Marekani isijaribu kuyawekea vikwazo mashirika ya nchi hiyo yanayofanya kazi nchini Venezuela.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema kuwa, hatua ya Washington ya kuyatishia mashirika ya Russia yanayofanya kazi nchini Venezuela ni ya kiburi. Imesisitiza kwamba iwapo vitisho hivyo vitafanyiwa kazi, basi Washington itapata jibu kali kutoka kwa Russia. Hivi karibuni, Marekani iliyaonya mashirika ya Russia yanayoendesha shughuli zake katika sekta ya mafuta nchini Venezuela kwamba iwapo yataendeleza shughuli hizo, yatawekewa vikwazo.

Vikwazo ni juhudi ya mwisho ya Marekani iliyofeli nchini Venezuela

Jumatatu iliyopita, Wizara ya Hazina ya Marekani iliiwekea vikwazo benki moja ya Russia ya Evrofinance Mosnarbank. Taarifa iliyotolewa na Washington ilidai kwamba uamuzi huo ulichukuliwa kufuatia benki hiyo kupindisha vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Venezuela. Inafaa kuashiria hapa kuwa mbali na Marekani kuiwekea vikwazo sekta ya mafuta ya Venezuela, pia ilifungia fedha za sekta hiyo zilizoko nchini humo na katika nchi nyingine za Magharibi.

Tags