Russia yapinga madola ya nje kuingilia masuala ya ndani ya Algeria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i52275-russia_yapinga_madola_ya_nje_kuingilia_masuala_ya_ndani_ya_algeria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Seregei Lavrov amesisitiza kuwa nchi yake inapinga uingiliaji wa madola ya nje katika masuala na hali inayoendelea hivi sasa nchini Algeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 19, 2019 23:02 UTC
  • Russia yapinga madola ya nje kuingilia masuala ya ndani ya Algeria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Seregei Lavrov amesisitiza kuwa nchi yake inapinga uingiliaji wa madola ya nje katika masuala na hali inayoendelea hivi sasa nchini Algeria.

Lavrov ametoa sisitizo hilo mjini Moscow akiwa na waziri mwenzake wa Algeria  Abdelkader Messahel, ambapo mbali na kueleza wasiwasi alionao kuhusu hali ya kisiasa ya Algeria ametahadharisha kuhusu njama za kutaka kuvuruga uthabiti ndani ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza upinzani wa Moscow wa madola ya nje kuingilia kwa namna yoyote ile masuala ya ndani ya Algeria na kuongeza kwamba: Tunashuhudia hatua kadhaa zinazochukuliwa ili kuifanya hali ya mambo iwe mbaya zaidi nchini Algeria; hatua hizo hazikubaliki.

Sergei Lavrov amebainisha kuwa, wananchi wa Algeria inapasa wao wenyewe waamue kuhusu hatima ya nchi yao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov (kulia) na mwenzake wa Algeria Abdelkader Messahel 

Amesema, nchi nyingi za eneo la kaskazini mwa Afrika zinataabika na kuatilika kutokana na uingiliaji wa madola ya nje katika masuala yao ya ndani.

Licha ya Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria kutangaza uamuzi wa kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania urais, maandamano ya upinzani yangali yanaendelea nchini humo huku wapinzani wake wakitaka yafanyike mageuzi ya msingi.

Siku ya Jumatatu, kiongozi huyo alisema kuwa, Algeria inakaribia kuingia kwenye mabadiliko ya utawala kwa njia ya mazungumzo jumuishi ya kitaifa yatakayofanyika muda si mrefu ujao kwa kushirikisha makundi yote nchini humo.../