Wamarekani waandamana kupinga kushambuliwa kijeshi Venezuela
(last modified Sun, 31 Mar 2019 07:41:51 GMT )
Mar 31, 2019 07:41 UTC
  • Wamarekani waandamana kupinga kushambuliwa kijeshi Venezuela

Mamia ya wananchi wa Marekani wamefanya maandamano mjini Washington DC kupinga uingiliaji wa aina yoyote wa kijeshi wa nchi hiyo dhidi ya Venezuela.

Marekani imekuwa ikisisitiza kuwa iko tayari kutumia njia ya kijeshi dhidi ya serikali halali ya Rais Nicolás Maduro. Bango moja kubwa lililokuwa limebebwa na waandamanaji hao lilikuwa na ujumbe usemao "Hapana kwa Vita! Hapana kwa NATO! Hapana kwa Vita Venezuela!"

Waandamanaji hao walikusanyika nje ya Ikulu ya Marekani White House, nje ya ofisi za Mfuko wa Fedha wa Kimataifa IMF, nje ya makao makuu ya Benki ya Dunia na karibu na ofisi za Jumuiya ya Mataifa ya Amerika OAS, huku wakipiga nara za kupinga kile walichokiita sera za kibeberu za Wamagharibi.

Mmoja wa waandamanaji hao, Alejandro Alvarez amesema fedha ambazo Marekani inataka kuzitumia katika kuishambulia kijeshi Venezuela zinapaswa kuelekezwa katika sekta ya elimu na afya.

Trump, makamu wake Pence, bintiye Ivanka na mke wa Juan Guaido katika Ikulu ya White House

Ikumbukwe kuwa mnamo Januari 23, kiongozi wa upinzani Juan Guaido alijitangaza kuwa rais wa Venezuela na punde baada ya hapo Marekani na baadhi ya madola ya Magharibi yalitangaza kumtambua. Wananchi wa Venezuela na wanajeshi wa nchi hiyo pamoja na nchi nyingi na muhimu duniani kama vile Russia, China, Afrika Kusini, Iran na Uturuki zimepinga hatua hiyo sanjari na kutangaza kumuunga mkono kikamilifu Rais Maduro.

Kadhalika waandamanaji hao katika mji wa Washington wamekosoa vikali kufanyika mkutano ujao wa ngazi ya mawaziri wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) katika mji huo mkuu wa Marekani. Mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa NATO unafanyika kuanzia Aprili 3 hadi 4.

Tags