Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela: Inatupasa kujifunza kutoka Iran
(last modified Wed, 08 May 2019 01:24:00 GMT )
May 08, 2019 01:24 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela: Inatupasa kujifunza kutoka Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela sambamba na kusisitiza umuhimu wa kupanua ushirikiano katika uga wa kijeshi na nishati kati ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kuwa Caracas inapaswa kujifundisha masomo mengi kutoka Iran.

Jorge Arreaza aliyasema hayo Jumanne ya jana akiwa mjini Moscow, Russia wakati wa mazungumzo na Shirika la Habari la IRNA kuhusiana na umuhimu wa kupanuliwa ushirikiano kati ya Iran na Venezuela na kuongeza kwa kusema: "Tunatakiwa tujifunze mambo mengi kutoka kwa Wairani kuhusu jinsi katika kipindi cha miongo kadhaa wameweza kustawisha uchumi wao licha ya vikwazo vya Marekani." Kadhalika Arreaza ameongeza kwamba kwa sasa nchi za Amerika ya Latini zikiwemo Venezuela, Cuba na Nicaragua ziko chini ya vikwazo na mzingiro wa kiuchumi wa Marekani, hivyo zinatakiwa kukabiliana kwa pamoja na hatua hizo za upande mmoja za Washington dhidi yao.

Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela

Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela sambamba na kusisitiza kwamba uhusiano wa Venezuela na Iran kwa muda wote umekuwa mzuri na kwamba hata katika serikali tofauti pia mahusiano hayo yameendelea kuimarika, ameongeza kwamba kwa sasa marais wa nchi mbili Nicolás Maduro na Hassan Rouhani wako katika kuboresha ushirikiano wa nchi zao. Inafaa kuashiria kuwa, katika siku za hivi karibuni Marekani na washirika wake wameongeza mashinikizo na njama zao kwa ajili ya kuing'oa madarakani serikali halali ya Venezuela ambayo ina msimamo ulio kinyume na jinsi Marekani inavyotaka.

Tags