Russia na Hamas zafanya mazungumzo mjini Moscow
(last modified Wed, 17 Jul 2019 07:43:18 GMT )
Jul 17, 2019 07:43 UTC
  • Russia na Hamas zafanya mazungumzo mjini Moscow

Ujumbe wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS umekutana mjini Moscow na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Mikhail Bogdanov ambapo pande mbili zimesisitizia umuhimu wa umoja wa Wapalestina kwa shabaha ya kuzima njama ya Marekani iliyopewa jina la Muamala wa Karne.

Ubalozi wa Russia mjini Tel Aviv umeripoti kuwa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Mikhail Bogdanov amefanya mazungumzo na mkuu wa ujumbe wa HAMAS, Mousa Abu Marzook, ambapo wamebadilishana mawazo pia kuhusu hali ya vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Hali kadhalika pande mbili hizo zimeeleza bayana kuwa, hakuna mbadala wa suluhu ya kisiasa katika kadhia ya Palestina.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema serikali ya Moscow iko tayari kuongoza jitihada za kupatikana umoja na mshikamano miongoni mwa mirengo hasimu ya kisiasa ya Palestina.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Mikhail Bogdanov

Russia imekuwa ikisisitiza kuwa, mpango wa Muamala wa Karne wa Marekani hautakuwa na natija yoyote katika mgogoro wa Palestina na utawala haramu wa Israel, na yumkini utavuruga zaidi mambo.

Wapalestina na viongozi wa nchi mbalimbali duniani wameupinga na kuukosoa vikali Muamala wa Karne, wakisisitiza kuwa hauna maslahi kwa Wapalestina, na ni njama ya Washington ya kutaka utawala za Kizayuni wa Israel utambulike na ukubalike katika uga wa kimataifa.

Tags