Russia: Iran imekusudia kupunguza tena utekelezaji wa majukumu yake katika JCPOA
Mjumbe mwandamizi wa timu ya Russia katika kikao cha kamisheni ya pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kilichofanyika mjini Vienna amesema, Iran ina mpango wa kuanza awamu mpya ya kupunguza utekelezaji wa ahadi na majukumu yake katika makubaliano hayo.
Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia na mkuu wa ujumbe wa nchi hiyo katika kikao cha kamisheni ya pamoja ya JCPOA, ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Interfax mwishoni mwa kikao hicho hapo jana na kuongeza kuwa: Kutokana na hali hiyo, washiriki wa kikao cha Vienna wamekubaliana kuwa jitihada zinazohitajika lazima zifanyike kuhakikisha Tehran inanufaika na faida za kiuchumi za makubaliano hayo ya nyuklia.
Ryabkov amebainisha kuwa, Russia itaendelea kushirikiana na Iran katika miradi iliyoainishwa katika JCPOA.
Kwa kutumia vifungu vya 26 na 36 vya JCPOA, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hadi sasa imeshapunguza katika awamu mbili baadhi ya majukumu yake iliyojikubalisha katika makubaliano hayo ya nyuklia kuhusiana na kiwango na uzito wa urani inayorutubisha; na sambamba na kutoa muhula mwingine wa siku 60 imesisitiza kuwa, endapo pande nyingine husika katika JCPOA zitaendelea kupuuza kutekeleza ahadi na majukumu yao, nayo pia itachukua hatua nyingine zaidi za kupunguza utekelezaji wa majukumu yake.
Akizungumza hapo jana baada ya kikao cha kamisheni ya pamoja ya JCPOA mjini Vienna, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran Sayyed Abbas Araqchi alisema, kikao hicho kimemalizika kwa mafanikio japo hatuwezi kusema kuwa mambo yote yametatuliwa.../