Mkuu wa Instex ajiuzulu, sababu, kuikosoa Israel
Gazeti la Bild linalochapishwa nchini Ujerumani limeripoti kuwa mkuu wa mfumo maalumu wa mabadilishano ya fedha kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya, kwa kifupi INSTEX, Bernd Erbel amejiuzulu wadhifa huo.
Gazeti hilo limeandika kuwa, Bernd Erbel amejiuzulu baada ya kufichuliwa mazungumzo yake na kituo kimoja cha redio akikosoa sera za ukandamizaji za utawala wa Kizayuni wa Isarel dhidi ya watu wa Palestina na kile kinachodaiwa ni mauaji ya mamilioni ya Wayahudi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, Holocaust.
Katika mahojiano hayo, Bernd Erbel pia alisema kuwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baina ya nchi za kundi la 5+1 na Iran ulikuwa uamuzi wa Ujerumani uliokuwa kinyume na matakwa ya utawala wa Kizayuni na kwamba Israel iliundwa kwa thamani ya kuwafukuza Wapalestina katika ardhi na nchi yao.
Tarehe 31 Januari mwaka huu Umoja wa Ulaya na baada ya miezi kadhaa ya majadiliano na Tehran, hatimaye ulianzisha mfumo huo maalumu wa kibiashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliopewa jina la INSTEX ingawa tangu wakati huo EU imekuwa ikichelewesha utekelezwaji wa mfumo huo kwa visingizio mbalimbali.

Makao makuu ya ofisi ya INSTEX ni Ufaransa, na Ujerumani imepewa jukumu la utekelezaji wake huku Uingereza ikiwa msimamizi wa mfumo huo.