Serikali ya Venezuela yasimamisha mazungumzo na wapinzani kulalamikia vikwazo vya Marekani
(last modified Sat, 10 Aug 2019 01:17:55 GMT )
Aug 10, 2019 01:17 UTC
  • Serikali ya Venezuela yasimamisha mazungumzo na wapinzani kulalamikia vikwazo vya Marekani

Marekani ikiwa ni nchi inayoingilia wazi wazi masuala ya ndani ya Venezuela imefanya juhudi nyingi za kuipigisha magoti serikali ya mrengo wa kushoto ya nchi hiyo na pia kujaribu kumng'oa madarakani Rais Nicolas Maduro wa nchi hiyo lakini bila mafanikio yoyote.

Hatua ya chuki na uhasama ya hivi karibuni kabisa ya Washington dhidi ya serikali hiyo halali iliyochaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Venezuela imetimia kwa kuwekewa nchi hiyo vikwazo vikali na vya pande zote. Hatua hiyo ya uadui ya watawala wa Marekani dhidi ya viongozi halali wa Venezuela imekabiliwa na radiamali ya viongozi wa serikali ya Caracas ambao wamesimamisha mazungumzo na wapinzani wa serikali. Duru ya pili ya mazungumzo hayo ilikuwa imepangwa kufanyika siku za Alkhamisi na Ujumaa iliyopita nchini Barbados. Akizungumzia suala hilo kupitia ujumbe wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Jorge Rodríguez, Waziri wa Habari wa Venezuela alisema Alkhamisi kwamba Rais Nicolas Maduro wa nchi hiyo alikuwa amechukua uamuzi wa kutotuma ujumbe wa Venezuela katika mazungumzo ya Barbados kwa lengo la kulalamikia hujuma ya kinyama na kidhalimu ya serikali ya Trump ya kuizingira Venezuela kiuchumi, kibiashara na kifedha kinyume cha sheria. Hata hivyo amesisitiza kwamba serikali ya Caracas iko tayari kutazama upya njia za kufanya mazungumzo na wapinzani kwa manufaa ya watu wa Venezuela.

Jorge Rodríguez, Waziri wa Habari wa Venezuela

Mzungumzo hayo yamesimamishwa na serikali katika hali ambayo tayari ujumbe wa wapinzani wanaoongozwa na Juan Guaido aliyejitangaza kuwa raia wa nchi hiyo tayari ulikuwa umewasili nchini Barbados kwa ajili ya kushiriki mazungumzo hayo. Wiki iliyopita Rais Nicolas Maduro wa Venezuela alitangaza rasmi kuanza mazungumzo hayo kwa shabaha ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini. Tarehe 8 Julai mwaka huu duru nyingine ya mazungumzo hayo ya amani ilifanyika katika kisiwa hicho hicho cha Barbados kwa upatanishi wa serikali ya Norway. Wakati hou Rais Maduro alisema kuwa mazungumzo hayo yalikuwa jumuishi ambayo yangeleta matumaini ya kufikiwa utatuzi wa mwisho wa mzozo wa nchi hiyo. Mwezi Mei mwaka huu pia duru nyingine mbili za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yalifanyika na wapinzani huko Oslo, kwa upatanishi wa serikali ya Norway.

Bila shaka vikwazo vya pande zote vya serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Venezuala ambavyo vinajumuisha kutaifishwa mali za taifa la Venezuela zilizoko nchini Marekani na pia mashirika ya nchi hiyo kukatazwa kufanywa biashara au kuwa na uhusiano wowote na Venezuela, vinatekelezwa kwa dhana kuwa hatimaye vitamlazimsiha Rais Maduro akubali kuondoka madarakani. Vikwazo hivyo si tu kuwa vinayazuia mashirika ya Marekani kufanya biashara na serikali ya Venezuela bali vinawacha wazi mlango wa kuwekewa mashinikizo na vikwazo mashirika na raia wa nchi nyingine ambao wataamua kufanya biashara na nchi hiyo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Venezuela siku ya Jumanne ilitoa taarifa ikitangaza kuwa: Vikwazo vipya vilivyotangazwa na serikali ya Donald Trump, ni mjumuiko mpya wa hatua za upande mmoja za ugaidi wa kiuchumi dhidi ya watu wa Venezuela.

Marekani inadhani kwamba kwa kutekeleza vikwazo vikali dhidi ya Venezuela na kulishinikiza jeshi, hatimaye itaweza kulilazimisha jeshi hilo lisimamishe uungaji mkono wake kwa serikali ya Rais Nicolas Maduro. Kusiana na suala hilo, Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa anasema kwamba vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Venezuela ni vikali na vingi mno na kuna uwezekano vikaharibu zaidi maisha ya mamilioni ya watu wa nchi hiyo kuhusiana na suala zima la kupata chakula na huduma za afya na tiba.

Michelle Bachelet, Kamisna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa

Inaonekana kuwa hatua ya serikali ya Trump ya kutaka kuiangusha serikali halali ya Venezuela vimeingia katika hatua mpya. Ni wazi kuwa hatua hiyo ya chuki imechukuliwa kutokana na kukata tamaa Trump kuhusiana na kushindwa wapinzani kuiangusha serikali ya Maduro na wakati huohuo ukakamavu mkubwa ulioonyeshwa na serikali ya Venezuela mbele ya mashinikizo makubwa na ya pande zote ya Marekani na muhimu kuliko yote, uungaji mkono wa watu wa Venezuela kwa serikali yao inayoongozwa na Maduro. Kwa kweli baada ya kushinfwa Trump kuiangusha serikali ya mrengo wa kushoto ya Caracas, sasa Marekani imeamua kutekeleza vikwazo vya pande zote na kuingilia moja kwa moja mambo ya ndani ya Venezuela. Hata hivyo hatua iliyochukuliwa hivi karibuni na serikali ya Caracas ni onyo kali kwa serikali ya Washington kwamba isidhani kuwa imefanikiwa kuitumbukiza Venezuela katika mtego wa kutaka kumpindua Rais Maduro wa nchi hiyo.

 

Tags