WHO yazitaka nchi zote kupiga marufuku matangazo ya sigara
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa wito wa kupigwa marufuku matangazo ya sigara katika matukio mbalimbali ya kimataifa.
Taarifa iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani imezitaka nchi zote kufuata maagizo ya Makubaliano Kupambana na Sigara na Tumbaku kwa kuacha kutangaza sigara katika maonyesho na mikutano ya kimataifa. Vilevile imezitaka nchi zote kuzuia udhamini wa kifedha wa makampuni mbalimbali wa bidhaa za tumbako na sigara.
Taarifa ya WHO imesisitiza kuwa: Dunia inapaswa kukomesha harakati ya kutangaza biashara ya sigara na bidhaa za tumbaku ambayo ndio chanzo cha mashaka na vifo vya mamilioni ya wanadamu wanaopoteza maisha kila mwaka. Taarifa hiyo imesema: Badala yake, nchi mbalimbali zinapaswa kufanya jitihada za kuimarisha afya na kulinda vizazi vijavyo na kupunguza idadi ya wavutaji wapya wa sigara.
Kifungu nambari 5.3 cha Makubaliano ya Kimataifa ya Kupambana na Sigara kinajumuisha wajibu wa kusaidia sera za kuimarisha afya ya umma katika uwanja wa kupambana na sigara mkabala wa maslahi ya kibiashara ya sekta hiyo. Makubaliano hayo pia yanayapiga marufuku makampuni kudhamini bidhaa za sigara katika maonyesho na mikutano ya kimataifa.
Takwimu za za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa watu milioni 8 wanaaga dunia kila mwaka kutokana na kutumia sigara moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja.