Maafa ya wakimbizi yaendelea kushuhudiwa Bahari ya Mediterania
Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM) limetangaza katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba, maafa ya wahajiri yanaendelea kushuhudiwa katika maji ya Bahari ya Mediterania.
Ripoti mpya ya shirika la IOM imesema kuwa, katika kipindi cha miezi 9 iliyopita ya mwaka huu wa 2019 wahajiri wasiopungua 1041 waliokuwa njiani kuelekea Ulaya hususan Italia kupitia Bahari ya Mediterania wakikimbia vita na ukatili katika nchi zao, wameaga dunia.
Awali Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa ilikuwa imetangza kuwa, katika mwaka uliopita wa 2018 wakimbizi zaidi ya elfu mbili walifariki dunia baada ya kuzama katika Bahari ya Mediterania.
Idadi kubwa ya wahajiri hao ambao ni kutoka nchi za magharibi mwa Asia na kaskazini mwa Afrika, wamekuwa wakikimbia nchi zao kutokana na vita, njaa na hali mbaya ya uchumi na kuelekea Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania.
Wachhambuzi wa mambo wanasema mgogoro mkubwa wa wahajiri na wakimbizi dunia ni matokeo ya siasa za uingiliaji kati za madola ya Magharibi katika nchi za eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika.