Kujitoa Trump katika JCPOA; ni katika kuiunga mkono Israel
Rais wa Marekani amekiri kuwa alijitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa sababu ya kuiunga mkono Israel.
Akihutubia kikao cha kila mwaka cha wanaharakati wa masuala ya kijamii wa Kihafidhina huko Washington, Donald Trump amebainisha kuwa, yeye ametambua rasmi umiliki wa Israel huko Golan na kujitoa katika makubaliano ya nyuklia na Iran. Rais wa Marekani amedai katika kikao hicho kwamba, Marekani itaendelea kuiunga mkono Israel na katika uwanja huo, wameuhamishia huko Quds ubalozi wa Marekani na kuutambua rasmi mji huo kama mji mkuu wa milele wa utawala wa Israel.
Trump amesema kuwa amejitoa kwenye makubaliano ya JCPOA ikiwa ni katika kuiunga mkono Israel ambapo huko nyuma pia, Rais huyo wa Marekani aliwahi kusema kuwa makubaliano hayo hayana manufaa yoyote kwa wananchi wa Marekani.
Rais Donald Trump tarehe Nane Mei mwaka jana alitangaza kujitoa rasmi ndani ya JCPOA na kurejesha tena vikwazo vya kiuhasama dhidi ya Iran.
Katika kukaribia uchaguzi wa rais nchini Marekani; wagombea wa kiti hicho wanapasa kuonyesha uungaji mkono wao kwa utawala wa Israel ili nao waungwe mkono na lobi za matajiri wa Kizayuni. Gharama za kuendeshea uchaguzi nchini Marekani ni kubwa mno kiasi kwamba, wagombea wa kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2016 walitumia zaidi ya dola bilioni moja katika kampeni zao za uchaguzi; fedha ambazo zilitolewa na lobi za Wazayuni.