Rais Rouhani: Kupenda vita Marekani kumechochea moto wa ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i56850-rais_rouhani_kupenda_vita_marekani_kumechochea_moto_wa_ugaidi
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akihutubia mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM, amesema kuwa siasa za upande mmoja za Marekani ndio sababu kuu ya kuibuka ugaidi katika maeneo tofauti ya dunia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 25, 2019 10:59 UTC
  • Rais Rouhani: Kupenda vita Marekani kumechochea moto wa ugaidi

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akihutubia mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM, amesema kuwa siasa za upande mmoja za Marekani ndio sababu kuu ya kuibuka ugaidi katika maeneo tofauti ya dunia.

Rais Rouhani ambaye anashiriki mkutano wa 18 wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungama na Siasa za Upande Wowote mjini Baku, mji mkuu wa Azerbaijan amesema kuwa, vita endelevu vya Marekani vimezisababishia nchi tofauti hasara ya mabilioni ya dola sambamba na kuibua fitina na ugaidi. Ameongeza kwamba Jumuiya ya Nchi Zisizofungama na Siasa za Upande wowote NAM kupitia uungaji mkono wa jamii kubwa na kutokana na ukubwa wake wa kijografia katika jamii ya kimataifa, inaweza kwa urahisi kuanzisha mrengo mpya wenye nguvu duniani. Kadhalika Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria machafuko ya hivi karibuni katika eneo na kusema, njia pekee ya kuepukana na migogoro hiyo, ni kuheshimu haki za mataifa katika kujiainishia mustakbali wao, kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kuandaliwa uwanja unaofaa kwa ajili ya ushirikiano na mazungumzo.

Watawala wa Marekani na washirika wao ndio waanzilishi wa ugaidi duniani

Akizungumzia suala la kudhamini usalama wa eneo amebainisha kwamba, katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa UNGA, Iran iliwasilisha pendekezo la 'Hatua ya Amani ya Hormoz' kwa ajili ya usalama na uthabiti katika eneo, lengo lake likiwa ni kukuza kiwango cha usalama, uthabiti, maendeleo, kuanzisha maelewano ya pande kadhaa na mahusiano ya amani na urafiki wa nchi za Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormoz. Rais Hassan Rouhani amesema kuwa Iran inaamini kwamba uthabiti na usalama wa majirani, uthabiti na usalama wa dunia na kupatikana usalama na maendeleo ya eneo ni mambo ambayo yatafikiwa tu kupitia ushirikiano na ushiriki wa majirani wote. Kando na mkutano wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungama na Siasa za Upande wowote NAM, Rais wa Iran amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi tofauti wanachama wa jumuiya hiyo mjini Baku.