Bangladesh yashikilia hukumu ya kifo dhidi ya Azharul Islam
Mahakama ya Juu ya Bangladesh imeidhinisha hukumu ya kifo iliyotolewa mwaka 2014 dhidi ya kinara wa chama cha Kiislamu cha Jamaat-e-Islami, A T M Azharul Islam, kwa tuhuma za kutenda jinai za kivita.
Majaji wa mahakama hiyo wakiongozwa na Jaji Mkuu, Syed Mahmud Hossain wametupilia mbali rufaa iliyowasilishwa na wakili wa kinara huyo, Khandker Mahbub Hossain, na hivyo kuandaa mazingira ya kutekelezwa hukumu ya kunyongwa Islam mwenye umri wa miaka 67.
Mmoja wa waendesha mashitaka wa serikali ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, yumkini Islam akanyongwa ndani ya miezi michache ijayo.
Islam atakuwa kiongozi wa sita wa ngazi za juu wa chama hicho kikubwa cha Kiislamu kuhukumiwa kifo kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita wakati wa harakati za kupigania uhuru mwaka 1971.
Islam ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama cha Jamaat-e-Islami alihukumiwa kunyongwa mwaka 2014 baada ya mahakama kusema kuwa imempata na hatia ya mauaji, ubakaji na mauaji wa kimbari wakati wa mgogoro na mapigano ya miezi tisa ambayo yalipelekea Bangladesh ijitenge na Pakistan.
Kinara huyo chama cha Kiislamu anadaiwa kuhusika na mauaji ya watu 1,200 katika wilaya ya Rangpur, kaskazini mwa nchi. Mawakili wa Islam wanasisitiza kuwa, tuhuma zote dhidi ya kiongozi huyo wa Jamaat-e-Islami ni bandia na kubambikiwa.