Marekani yaanza kujiondoa rasmi kwenye Makubaliano ya Paris
(last modified Tue, 05 Nov 2019 07:23:07 GMT )
Nov 05, 2019 07:23 UTC
  • Marekani yaanza kujiondoa rasmi kwenye Makubaliano ya Paris

Marekani imeanzisha mchakato wa kujiondoa rasmi katika makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi yaliyofikiwa mjini Paris, Ufaransa mwaka 2015.

Mchakato huo unatazamiwa kukamilika kufikia Novemba 4 mwaka ujao 2020, siku moja baada ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini Marekani, ambapo Rais Donald Trump anatazamiwa kugombea muhula wa pili.

Mwaka 2017, Trump alitangaza kuiondoa Marekani  katika muafaka huo wa kimataifa, akisisitiza kuwa makubaliano hayo hayana faida yoyote kwa nchi yake.

Weledi wa mambo wanaamini kwamba, hatua ya Marekani ya kujiondoa katika mkataba huo itaisababishia sayari ya dunia ongezeko kubwa la joto kali, hasa kwa kuzingatia kuwa, Marekani ndio chanzo kikuu cha kuongezeka joto hilo dunia. 

Maandamano ya kupinga misimamo ya Trump kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa nje ya White House

Kwa mtazamo wa rais huyo wa Marekani, kimsingi suala la ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi ni mambo yasiyo na ukweli wowote na kwamba eti mambo hayo yamebuniwa tu na Wachina.

Katika hatua nyingine, utafiti mpya uliofanywa na taasisi ya Tata Centre for Development ya Chuo Kikuu cha Chicago umeonyesha kuwa, kufikia mwisho wa karne hii ya 21, watu milioni moja na laki moja watakuwa wanafariki dunia kila mwaka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini India.