Shirika la FAO lasisitiza kuimarisha uhusiano na Iran
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesisitizia azma yake ya kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati yake na Iran.
Qu Dongyu, Mkurugenzi Mkuu wa FAO amesisitizia haya ya kuimarishwa ushirikiano wa pande zote kati ya shirika hilo na Iran na kueleza kuwa uhusiano mzuri wa pande mbii uliokuweko huko nyuma ni wazi utaandaa uwanja mzuri wa ushirikiano mkubwa zaidi kati ya FAO na Iran.
Ushirikiano huo utakuwa na matokeo chanya kwa wakulima wa Iran na kupelekea kustawika zaidi maeneo ya vijijini humu nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni moja nchi wanachama hai wa FAO ambayo ina ushirikiano wa karibu na shirika hilo katika kufanikisha malengo ya ustawi endelevu hususan kutokomeza njaa na kuhakikisha usalama wa chakula unakuwepo duniani.
Shirika la Chakula na Kilimo Duniani liliasisiwa katika mji mkuu wa Italia mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia kwa lengo la kuendeleza kilimo na kutatua matatizo ya chakula ulimwenguni. Qu Dongyu ambaye alichaguliwa miezi mitano iliyopita kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la FAO katika duru ya kwanza ya uchaguzi kwa kupata kura nyingi za wajumbe wa nchi mbalimbali duniani licha upinzani mkubwa wa Marekani; ameagiza kutekelezwa mkakati wa kivitendo alioupa jina la " Mkono kwa Mkono" baada ya kupita miezi miwili ya kukalia kiti hicho cha Mkurugenzi Mkuu lengo likiwa ni ikuboresha usalama wa chakula duniani.