Dec 04, 2019 07:08 UTC
  • HRW: Bangladesh inawanyima elimu watoto laki 4 wa Kirohingya

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema serikali ya Bangladesh imewanyima haki ya kupata elimu watoto laki nne Waislamu Warohingya wanaoishi kama wakimbizi nchini humo.

Shirika hilo lenye makao makuu yake mjini New York limesema hayo katika ripoti yake ya kurasa 81 iliyotolewa jana Jumanne, yenye anwani inayosema: Je, sisi sio Wanadamu? Kunyimwa Elimu Watoto Wakimbizi wa Rohingya nchini Bagladesh.

Bill Van Esveld, Mkurugenzi wa Haki za Watoto wa Human Rights Watch amesema, "Bangladesh imetangaza wazi kuwa inataka kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Rohingya, lakini kuwanyima watoto haki ya elimu kunawaumiza watoto hao na kitendo hicho kinawazidishia majanga na machungu wakimbizi Warohingya."

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, serikali ya Dhaka mbali na kukataa watoto hao wapewe elimu rasmi, pia imeyakataza mashirika ya kiraia kutumia mtaala usio rasmi wa Bangladesh kuwapa elimu watoto hao wanaoshi kambini, ikisisitiza kuwa, wakimbizi hao wataondoka nchini na kurejea makwao ndani ya miaka miwili.

Waislamu wakimbizi wa Rohingya wanaopitia mazito Bangladesh

Mnamo 25 Novemba 2018, Bangladesh na Myanmar zilitiliana saini mapatano ya kuwawezesha wakimbizi Waislamu Warohingya kurejea katika makao yao mkoani Rakhine lakini utawala wa Myanmar umeweka vizingiti katika utekelezwaji wa mapatano hayo.

Itakumbukwa kuwa tarehe 25 Agosti 2017 jeshi la Myanmar kwa kushirikiana na Mabudha wenye misimamo ya kigaidi lilianzisha mauaji makali dhidi ya Waislamu wa Rohingya katika mkoa wa Rakhine, magharibi mwa nchi ambapo zaidi ya Waislamu elfu sita waliuawa na wengine elfu nane kujeruhiwa. Aidha karibi Waislamu milioni moja wa jamii hiyo walikimbilia nchi jirani ya Bangladesh ili kuokoa maisha yao. 

Tags