Madai ya kipuuzi ya Marekani kuhusu kushadidisha vikwazo dhidi ya Iran
(last modified Wed, 01 Jan 2020 02:50:45 GMT )
Jan 01, 2020 02:50 UTC
  • Madai ya kipuuzi ya Marekani kuhusu kushadidisha vikwazo dhidi ya Iran

Katika kipindi cha utawala wa Rais Donald Trump, Marekani imeiwekea Iran vikwazo vikali ikiwa ni katika kutekeleza siasa zake za mashinikizo ya kiwango cha juuu kabisa.

Baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) Mei mwaka juzi 2018, iliiwekea vikwazo vikali kabisa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Licha ya kuwa siasa hizo za vikwazo hazijafua dafu, lakini Washington ingali imeng'ang'ania kushadidisha vikwazo.

Katika uwanja huo, Brian Hook, mkuu wa "Kundi la Uchukuaji Hatua Dhidi ya Iran" katika Wizara ya Mambo ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani, tarehe 30 ya mwezi uliopita wa Disemba alisema kuwa, katika mwaka huu mpya wa 2020, Marekani itaendeleza vikwazo vyake dhidi ya Iran na kwamba, vikwazo hivyo vitashadidishwa. Hook sambamba na kubainisha kwamba, yumkini Washington ikaongeza kiwango cha vikwazo vyake dhidi ya Iran amesema kuwa, Marekani imeridhishwa na athari hasi zilizoukumba uchumi wa Iran.

Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran

Brian Hook amedai kwamba, uchumi wa Iran umo katika hali ya kudhoofika na kwamba, kushadidishwa vikwazo dhidi ya Iran katika mwaka huu wa 2020 kutazidi kuudhoofisha uchumi huo. Mkuu huyo wa "Kundi la Uchukuaji Hatua Dhidi ya Iran" katika Wizara ya Mambo ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani ameeleza kuwa, hivi sasa ustawi wa uchumi wa Iran unakabiliwa na hali hasi, na endapo Tehran haitabadilisha siasa zake, basi uchumi wake utasambaratika.

Marekani imetangaza mara chungu nzima kwamba, lengo la kutumia wenzo wa 'mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa' dhidi ya Iran ni kufikia makubaliano mapya na Tehran ambapo katika makubaliano hayo masuala yote yanayoridhiwa na Marekani yazingatiwe. Serikali ya Trump imesisitiza mara nyingi kwamba, inatekelezwa vikwazo ambavyo havijawahi kushuhudiwa katika historia dhidi ya Iran ili kulilazimisha taifa hili lisalimu amri mbele ya matakwa haramu na yasiyo ya kisheria ya Washington.

Wamarekani wamepuuza kutokuwa na natija vikwazo hivyo na badala yake wameng'ang'ani msimamo wa kupiga ngoma ya vikwazo vya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Iran. Licha ya hatua hizo za chuki na uadui za Marekani, lakini Iran imesisitiza mara chungu nzima kwamba, haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya Washington.

Huko nyuma Marekani ilikuwa ikidai kwamba, inazingatia masuala ya haki za binadamu kuhusiana na vikwazo vyake dhidi ya Iran. Hata hivyo filihali imedhihirika wazi na bayana kwamba, uzingatiaji huo nao haupo. Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameashiria matamshi ya Rais wa Marekani anayezungumzia 'vita vya kiuchuumi' na kueleza kwamba, mimi ninauita huo kuwa ni 'ugaidi wa kiuchumi' kwa sababu hatua hizo zimewalenga wananchi wa kawaida.

Mtandao wa SRF wa Sweden umeandika: Marekani ikiwa na lengo la kuishinikiza Iran na nchi zote zinazoshirikiana nayo, imeiwekea vikwazo Tehran. Hata hivyo hatua hii imepelekea kutokea uhaba wa dawa na chakula nchini Iran na hivyo kuhatarisha maisha ya watu wengi hususan wagonjwa wanaougua maradhi ya saratani.

Kutokuwa na natija vikwazo visivyo vya kibinadamu vya Marekani vyenye lengo la kuishinikiza Tehran isalimu amri na kufuata matakwa ya Washington kumeifanya serikali ya Trump ifunue pazia kuhusiana na Iran na kushadidisha hatua zilizo dhidi ya ubinadamu dhidi ya wananchi wa taifa hili la Kiislamu.

Tags