Newsweek: Wanajeshi 270 wa Marekani wameuawa katika mashambulio ya SEPAH
Kwa mara ya kwanza toleo la mtandao la gazeti la kila wiki la Newsweek la Marekani limefichua kwamba, kwa uchache wanajeshi 270 wa nchi hiyo wameangamizwa katika shambulio la usiku wa kuamkia Jumatano lililofanywa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH katika kambi mbili za Marekani za Ain al Asad na Erbil nchini Iraq.
Kanali ya Kwanza ya Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza habari hiyo na kuongeza kwamba, gazeti hilo la Marekani limewanukuu askari wa nchi hiyo walioko lraq wakimsuta Donald Trump na kusema, rais huyo amesema uongo alipodai kwamba hakuna askari hata mmoja wa Marekani aliyeuawa wala kujeruhiwa katika shambulizi hilo la lran.
Hata hivyo dakika chache baadaye, habari hiyo imefutwa katika toleo hilo la mtandaoni la gazeti la Newsweek la Marekani lenye mfungamano na gazeti la New York Times. Huku hayo yakiripotiwa, mikanda mbalimbali ya video inaendelea kuenea kwenye mitandao ya kijamii inayoonesha jinsi makombora ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH yalivyokuwa yanapiga maeneo tofauti muhimu ya kambi ya kijeshi ya Ain al Asad ya Marekani nchini Iraq.

Kanali ya Kwanza ya Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imerusha hewani baadhi ya mikanda hiyo ya video ikionesha moto mkubwa uliokuwa unasababishwa na kila kombora la SEPAH lililokuwa linatua kwenye kambi ya Ain al Asad huku sauti za hofu, mayowe na kuomba msaada za wanajeshi wa Marekani zikisikika, ikiwa ni uthibitisho kwamba wanajeshi wa Marekani walikuwepo kwenye kambi hiyo tofauti na madai ya baadhi ya vyombo vya habari kwamba eti kambi hiyo ilikuwa tu na wanajeshi hao walikuwa wameshaondoka.
Habari nyingine zinsema kuwa, wananchi wa Syria wameviambia vyombo mbalimbali vya habari kwamba wameshuhudia msafara mrefu wa askari vamizi wa Marekani wakiondoka nchini humo baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH kutoa majibu makali kwa wanajeshi wa Marekani katika nchi jirani ya Iraq. Hatua hiyo ya kukimbia wanajeshi vamizi wa Marekani nchini Syria imekuja licha ya kwamba rais wa nchi hiyo Donald Trump juzi Jumatano alisisitiza tena kwamba hana nia ya kuondoa wanajeshi wake katika eneo lolote la Asia Magharibi.