Kutekelezwa utaratibu wa kutatua hitilafu katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA
(last modified Wed, 15 Jan 2020 12:52:19 GMT )
Jan 15, 2020 12:52 UTC
  • Kutekelezwa utaratibu wa kutatua hitilafu katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA

Nchi tatu za Ulaya zimeamua kutekeleza utaratibu wa kutatua hitilafu katika mapatano ya nyuklia ya Iran ambayo yanajulikana rasmi kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA).

Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, siku ya Jumanne zilitoa taarifa ya pamoja ambayo inaenda sambamba na sera zilizo dhidi ya Iran za Ikulu ya White House ambapo, bila kuashiria namna Marekani ilivyokiuka ahadi zake, taarifa hiyo imedai kuwa, "Kwa kuzingatia hatua za Iran, ambapo nchi hii haifungamani na ahadi zake katika JCPOA, tunalipeleka suala hilo mbele ya Kamati ya Pamoja." 

Pamoja na hayo Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya ametoa taarifa na kuashiria uamuzi wa nchi hizo tatu za Ulaya na kusema: "Lengo la mchakato huu ni kutafuta utatuzi wa masuala yanayohusu utekelezwaji wa mapatano katika fremu ya Kamati ya Pamoja." Aidha amesema ana matumani kuhusu lengo la mawaziri wa mambo ya nje katika kulinda JCPOA la kuondoa mkwamo uliopo kwa njia ya mazungumza ya kidiplomasia.

Mapatano ya nyuklia ya JCPOA yalifikiwa Julai mwaka 2015 baina ya Iran na kundi la 5+1 ambalo awali lilijumuisha Russia, China, Uingereza, Ufaransa, Marekani na Ujerumani na kisha kundi hilo likabadilika na kuwa 4+1 baada ya Marekani kujiondoa. Mapatano hayo yameweka wazi mbinu ya kuanzisha Tume ya Utatuzi. Kwa mujibu wa kipengee cha 36 cha mapatano ya JCPOA, iwapo Iran au nchi zingine katika JCPOA zitakuwa na malalamiko kuhusu upande mwingine kutofungamana na mapatano, basi Tume ya Utatuzi itaanza kufanya kazi.

Josep Borrell  Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya

Awali tume hiyo itaanza kufanya kazi kwa kuwashirikisha manaibu wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama na ikilazimika mawaziri wa mambo ya nje wataitisha kikao ili kuchunguza masuala yanayohusu ukiukwaji wa JCPOA. Aidha kwa mujibu wa kipengee hicho kunaweza kuundwa baraza la mashauriano litakalojumuisha wanachama watatu ambao watajumuisha upande unaolalamika na upande unaolalamikiwa na mwanachama mmoja asiye pendelea upande wowote. Baada ya mkutano wa pande hizo tatu, baraza hilo linaweza kutoa ushauri ambao si lazima utekelezwe. Hatimaye iwapo nchi yenye au zenye kulalamika hazitaridhika katika muda ulioainishwa, basi kadhia hiyo itapelekwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kipengee cha 37 cha JCPOA kimeweka wazi njia ya upigaji kura katika Baraza la Usalama na uwezekano wa kurejeshwa vikwazo vya umoja huo dhidi ya Iran na mchakato huo ni maarufu kama 'utaratibu wa ufyatuaji'.

Kwa maneno mengine ni kuwa, uamuzi wa nchi tatu za Umoja wa Ulaya wa kuanzisha Tume ya Utatuzi wa hitilaifu katika JCPOA unatafuatiana na 'utaratibu wa ufyatuaji. Tume hiyo inatazamiwa kuchunguza hitilafu zilizopo baina ya Iran na nchi tatu za Ulaya. Nchi za Ulaya zinadai kuwa, hatua ya Iran kupunguza hatua kwa hatua utekelezaji wa ahadi zake katika JCPOA ndio iliyoandaa mazingira ya kuundwa Tume ya Utatuzi wa Hitilafu. Hii ni katika hali ambayo, baada ya miezi kadhaa ya subira kufuatia hatua ya Marekani kukiuka mapatano na nchi za Ulaya kutochukua hatua za kivitendo kukabiliana na kitendo hicho cha Washington, Iran ilianza kuchukua hatua za kupunguza utekelezaji wa ahadi na majukumu yake katika JCPOA na ili kuwe na mliangano baina ahadi na haki zake. Kwa kujiondoa Marekani katika JCPOA, wakuu wa Washington walirejesha vikwazo vyao vya upande mmoja dhidi ya Iran na kwa msingi huyo ikakiuka maslahi ya Tehran katika JCPOA. Nchi za Ulaya nazo hazikuchukua hatua zozote za kivitendo za kufidia hasara ambazo Iran imepata kutokana na vikwazo hivyo vya Marekani.

Hivi sasa inaelekea kuwa, nchi za Ulaya kwa kutumia kipengee cha 36 cha JCPOA zinataka kuishinikiza Iran kutokana na hatua yake ya kupunguza utekelezaji wa ahadi zake katika JCPOA na kwa msingi huo kuandaa mazingira ya kutayarishwa mapatano mapya yatakayochukua sehemu ya JCPOA na hivyo kutekeleza takwa la rais Trump wa Marekani. Hii ni katika hali ambayo uzoefu wa miaka miwili iliyopita umeonyesha kuwa Iran hujibu mashinikizo kwa mashinikizo na haiwezi kulegeza msimamo kuhusu haki zake za kisheria. Kwa maelezo hayo, inatarajiwa kuwa, iwapo nchi za Ulaya zimeanzisha mchakato wa utatuzi katika JCPOA ili ziweze kufikia  'utaratibua wa ufyatuaji' na hivyo kurejeshwa vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya Iran, basi zitakabiliwa na jibu kali la Iran.

Tags