Mamia waandamana Tel Aviv na London kupinga 'Muamala wa Karne'
Mamia ya watu wamefanya maandamano katika barabara za mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, Tel Aviv kulaani "Muamala wa Karne" uliozinduliwa hivi karibuni na Rais Donald Trump wa Marekani, anayedai kuwa mapendekezo yaliyomo kwenye mpango huo ghalati yataleta suluhu ya amani ya mgogoro baina ya Israel na Palestina.
Shirika la habari la Iran Press limeripoti kuwa, waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yenye picha inayomuonyesha Trump akimkumbatia Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, ikiambatana na maneno yanayosema "Msiufanye mfumo wa ubaguzi wa rangi wa 'Apartheid' kuwa mkubwa tena."
Katika maandamano hayo ya jana usiku, waandamanaji hao wamesema njama hizo za Trump na Netanyahu zilizopewa jina la "Muamala wa Karne" zitawafanya Waarabu wenye uraia wa Israel kupokonywa uraia wao na kufukuzwa na kwamba mpango huo kiujumla hauna maslahi kwa yeyote.
Aidha maandamano mengine yalishuhudiwa jana katika mji mkuu wa Uingereza, London dhidi ya Mpango wa Muamala wa Karne uliozinduliwa Jumanne iliyopita na Rais Donald Trump wa Marekani na ambao unajumuisha kukabidhiwa kikamilifu Israel mji mtakatifu wa Quds wenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa na vitongoji vilivyoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Aidha mpango huo batili wa Trump unataka Wapalestina wasiwe na haki ya kurejea kwenye ardhi za mababu zao na makundi ya muqawama wa Palestina yapokonywe silaha ili kusiwe na jambo lolote linalohatarisha usalama wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Wananchi wa nchi mbalimbali duniani juzi Ijumaa walifanya maandamano makubwa kulaani mpango huo mpya wa Marekani wa kutaka kuwapora Wapalestina na Waislamu kiujumla maeneo yao matakatifu.