Louis Farakkhan amlaani Trump kwa kumuua Soleimani
Louis Farrakhan, kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya Nation of Islam ya nchini Marekani amemlaani vikali Rais Donald Trump wa nchi hiyo kwa kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, jenerali Muirani aliyekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ugaidi.
Katika hotuba yake hivi karibuni huko Detroit, Michigan, Farrakhan alisema: "Bw. Trump, umemuua Qassem Soleimani ambaye ni ndugu yangu."
Mwanaharakati huyo maarufu Mmarekani mwenye asili ya Afrika amelaani Trump kwa kujaribu kutetea ugaidi huo wa kumuua Jenerali Qassem Soleimani. Louis Farrakhan ameendelea kusema: "Bw. Trump…umedai kuwa ndugu yangu (Qassem Soleimani) ni gaidi...unaweza pia kuniita gaidi ili kesho uhalalishe kile ambacho serikali inapanga kukifanya dhidi yangu na Harakati ya Nation of Islam."
Louis Farraklhan amesema: "Mbinu unayoitumia wewe ni mauaji. Hapa nilipo unataka kunuia. Baada ya hotuba hii yamkini ukaharakisha njama yako hiyo."
Ikumbukwe kuwa Qassem Soleimani , Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye Januari 3 mwaka huu alielekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo aliuliwa shahidi akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq cha Hashd al Sha'abi na wanajihadi wengine wanane katika shambulio la kigaidi la jeshi la kigaidi la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad.