Putin asaini mpango wa kuifanyia marekebisho katiba ya Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i59757-putin_asaini_mpango_wa_kuifanyia_marekebisho_katiba_ya_russia
Suala la kuifanyia marekebisho katiba na mustakbali wa kisiasa wa Rais Vladimir Putin wa Russia ni jambo lililopewa uzito miongoni mwa matukio ya kisiasa ya karibuni huko Russia. Suala hilo linatazamiwa kuathiri pakubwa mustakbali wa Russia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 15, 2020 04:37 UTC
  • Putin asaini mpango wa kuifanyia marekebisho katiba ya Russia

Suala la kuifanyia marekebisho katiba na mustakbali wa kisiasa wa Rais Vladimir Putin wa Russia ni jambo lililopewa uzito miongoni mwa matukio ya kisiasa ya karibuni huko Russia. Suala hilo linatazamiwa kuathiri pakubwa mustakbali wa Russia.

Kuhusiana na suala hilo, Rais Vladimir Putin wa Russia jana Machi 14 alisaini mpango wa kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo. Kura ya maoni katika uwanja huo itafanyika baada ya Mahakama ya Katiba ya Russia kuidhinisha mfumo wa utekelezaji wa marebisho hayo ya katiba. Marekebisho yanayotazamiwa kutekelezwa katika katiba ya Russia yatapigiwa kura na yataweza kutekelezwa iwapo wananchi watayaunga mkono kwa  zaidi ya asilimia 50 ya kura.  

Tukio muhimu katika uwanja huo lilikuwa ni kupasishwa  na  kuongezwa vipengee vitakavyofanyiwa marekebisho ndani ya katiba ya Russia kupitia vikao vya bunge jambo lilimuandalia njia Putin ya kusalia madarakani baada ya kumalizika muda wake wa kisheria wa urais. Kwa mujibu wa marekebisho yaliyopasishwa; hakuna mtu atakayeruhusiwa kushikilia kiti cha rais kwa zaidi ya mihula miwili; ila hapa Rais wa sasa wa Russia Vladimir Putin anayo haki ya kuwa mgombea kwa mara nyingine hadi mwaka 2024.  

Bunge la Russia (Duma) Jumatano iliyopita Machi 11 lilipiga kura za ndio 383,  pasina kura za hapana, huku wabunge 42 wakijizuia kupiga kura na hivyo kuunga mkono pendekezo kuhusu kufanyiwa marekebisho katiba ya nchi hiyo na kuongezwa muhula wa uongozi wa Rais Vladimir Putin; pendekezo ambalo liliwasilishwa na mwanachama mwenzake. Wabunge 24 pia hawakuwepo wakati kura hiyo ikipigwa. Pendekezo hilo ambalo awali   lilikabiliwa na radiamali ya Putin lilikuwa limewasilishwa katika Duma ya Russia Januari 20 mwaka huu. 

Bunge la Russia (Duma)  

Baada ya kupasishwa rasimu ya kuifanyia marekebisho katiba ya Russia katika bunge la nchi hiyo; Baraza la Shirikisho la nchi hiyo siku hiyo hiyo nalo lilipasisha rasimu hiyo. Putin ameeleza kuwa ataidhinisha rasimu hiyo ya mabadiliko ya katiba na atagombea katika uchaguzi wa mwaka 2024 kama Mahakama ya Katiba pia itaafiki suala hilo na pia kuidhinisha muhula wake wa urais.

Hivi sasa Putin anaonekana kutazama upya msimamo wake wa huko nyuma kinyume na mwenendo na msimamo wake wa awali ambapo alitangaza rasmi kuwa anapinga kuongezwa kipindi chake cha urais baada ya kutangazwa marekebisho ya katiba.  

Rais Vladimir Putin wa Russia  

Kwa msingi huo mmoja wa wanachama wa chama tawala cha Russia cha United Russia amewasilisha bungeni kipengee kinachomruhusu Putin kugombea tena kiti cha rais katika uchaguzi wa mwaka 2024 na kupasishwa na bunge hilo. Tofauti na sera na mitazamo yake ya hapo awali, Putin kama kiongozi mwenye nguvu na taathira kubwa amefikia natija kwamba iwapo madaraka ya nchi yatashikwa na mwanasiasa mwingine katika uchaguzi rais mwaka 2024, yumkini hali ya mambo ikaenda kinyume kabisa na sera na mitazamo yake licha ya hatua alizochukua katika marekebisho ya katiba yanayomuwezesha kuendelea kuwa mtu mwenye athari kubwa katika siasa za Russia. 

Pamoja na hayo yote, uchunguzi wa maoni unaonyesha aghalabu ya wananchi wa Russia wanamuunga mkono Putin na wanamtaka aendelea kusalia madarakani. Putin amesema kuwa Russia inahitaji rais mwenye nguvu kwa kuzingatia ukubwa wa nchi hiyo, dini nyingi, idadi kubwa ya watu na jamii mbalimbali zinazoishi nchini humo. Putin akiwa Rais wa Russia amekuwa na mchango na nafasi muhimu sana katika matukio ya nchi hiyo katika miongo miwili iliyopita; na inatabiriwa kuwa kwa kuzingatia kuendelea duru yake ya urais hadi mwaka 2024, rais huyo si tu kuwa ataendeleza nafasi yake hiyo hadi wakati huo bali atakuwa na mchango mkubwa katika nchi hiyo kubwa duniani hata baada ya kumalizika muhula wake huo.