Mahakama ya Katiba ya Russia yapasisha sheria ya marekebisho ya Katiba
-
Vladimir Putin
Mahakama ya Katiba ya Russia imepasisha mapendekezo yaliyotolewa na Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin kwa ajili ya kurekebisha Katiba.
Taarifa iliyotolewa na Mahakama ya Katiba ya Russia imesema kuwa, mapendekezo ya Rais Rais Putin yatakayomuwezesha kubakia madarakani baada ya kumalizika muhula wa utawala wake wa sasa hayapingani na Katiba ya nchi.
Uamuzi huo wa majaji wa Mahakama ya Katiba ya Russia hauhitaji tena idhini ya chombo chochote cha dola.
Rais Vladimir Putin jana Jumamosi wiki hii aliidhinisha azimio lililopasishwa na Bunge la nchi hiyo kuhusu marekebisho ya Katiba ambayo yatarefusha kipindi cha uongozi wa rais wa sasa wa nchi hiyo baada ya kupigiwa kura ya maoni ya wananchi. Kura hiyo ya maoni ya kupasisha marekebisho hayo itafanyika tarehe 22 Aprili mwaka huu.
Bunge la Russia (Duma) Jumatano iliyopita Machi 11 lilipiga kura 383 za ndio, pasina kura za hapana, huku wabunge 42 wakijizuia kupiga kura na kupasisha muswada wa mapendekezo ya Putin.
Baraza la Shirikisho la Russia pia siku hiyo hiyo lilipasisha sheria hiyo inayomruhusu Putin kugombea tena urais mwaka 2024.
Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa, aghalabu ya wananchi wa Russia wanamuunga mkono Putin na wanamtaka aendelea kuongoza nchi hiyo.