Harakati za Palestina na Russia wakubaliana kukabiliana na "Muamala wa Karne"
(last modified Wed, 18 Mar 2020 06:24:01 GMT )
Mar 18, 2020 06:24 UTC
  • Harakati za Palestina na Russia wakubaliana kukabiliana na

Harakati za kupigania ukombozi wa Palestina zimekubaliana na Russia juu ya jinsi ya kukabiliana na mpango uliopendekezwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwa ajili eti ya amani Mashariki ya Kati maarufu kwa jina la "Muamala wa Karne".

Nayef Hawatmeh Katibu Mkuu wa Harakati ya Kidemokrasia kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina ameiambia televisheni ya al Mayadeen ya Lebanon kwamba, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amekutana na wawakilishi wa harakati za Palestina mjini Moscow ambako alitilia mkazo udharura wa kupatikana suluhisho la kisiasa la mgogoro wa Palestina kwa mujibu wa maazimio ya kimataifa.

Hawatmeh ameongeza kuwa, maafisa wa harakati za Palestina na wa Russia wamesema kuwa, mpango uliopendekezwa na Donald Trump wa Muamala wa Karne ni hatari kubwa kwa amani na usalama, unatayarisha mazingira ya kutokea machafuko zaidi na una madhara makubwa kwa mataifa yote ya Mashariki ya Kati.

Wapalestina wanapinga "Muamala wa Karne"

Katibu Mkuu wa Harakati ya Kidemokrasia kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina ameashiria umuhimu wa kufanyika uchaguzi katika eneo la Quds tukufu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kama sehemu ya ardhi mama ya Palestina na kusema kuwa, uchaguzi hauwezi kufanyika Palestina bina ya kushirikisha eneo hilo takatifu. 

Ujumbe wa harakati za ukombozi wa Palestina ulikuwa safarini Morscow kwa mwaliko wa serikali ya Russia.  

Tags