Kenya ni taifa lenye furaha zaidi Afrika Mashariki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i59898-kenya_ni_taifa_lenye_furaha_zaidi_afrika_mashariki
Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu furaha duniani imeitaja Kenya kuwa nchi yenye furaha zaidi katika eneo la mashariki ya Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 22, 2020 08:49 UTC
  • Kenya ni  taifa lenye furaha zaidi Afrika Mashariki

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu furaha duniani imeitaja Kenya kuwa nchi yenye furaha zaidi katika eneo la mashariki ya Afrika.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ambayo imetayarishwa na Mtandao wa Umoja wa Mataifa wa Suluhisho Kuhusu Maendeleo Endelevu,  pamoja na kuwa Kenya ni nchi yenye furaha zaidi Afrika Mashariki lakini katika orodha ya dunia haijafanya vizuri kwani imeorodheshwa ya 121 kati ya 156 ambazo zilichunguzwa.

Ripoti hiyo ya 8 ya Umoja wa Mataifa kuhusu furaha dunaini inaonyesha kuwa Kenya imepata pointi 4.583 kati ya pointi 10.

Baada ya Kenya nchi iliyoshika nafasi bora Afrika Mashariki ni Uganda ikiwa ya 126 ikifuatiwa na Burundi 140, Tanzania iko katika nafasi ya 148 duniani nayo Rwanda imeshika nafasi ya 150 huku  Sudan Kusini ikiwa  mwisho katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kushika nafasi ya 152 duniani na hivyo kuifanya kuwa mingoni mwa nchi za mwisho katika orodha hiyo.

Kwa mwaka wa tatu mfululizo, Finland imeorodheshwa kuwa nchi ambayo watu wake wana furaha zaidi duniani ambapo imepata  pointi 7.809 ikifuatiwa na Uswisi,  Iceland na Norway.

Vita Sudan Kusini vimepelekea watu wa nchi hiyo wawe miongoni mwa wasio kuwa na furaha  duniani

Libya imetajwa kuwa nchi ambayo  watu wake wana furaha zaidi Afrika baada ya kupata pointi 5.489 ikufuatiwa na Kodivaa, Benin, Jamhuri ya Kongo, Ghana, Morocco na Cameroon.

Vigezo ambavyo vimetumiwa na Umoja wa Mataifa kuainisha furaha ya watu katika nchi ni pamoja na Pato Ghafi la Taifa au GDP, himaya ya kijamii kwa raia, matumaini ya uhai,  uhuru wa maamuzi ya kimasiha, ukarimu, na ukosefu wa ufisadi na ubadhirufu wa fedha za umma.