Seneta wa Marekani aionya Saudia kwa kushusha bei ya mafuta
Seneta wa chama cha Republican nchini Marekani ameitahadharisha Saudia kuhusu kushuka kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia kutokana na tofauti zake na Russia na kuitaka ibadili mienendo yake.
Kevin Cramer ameyasema hayo kwenye ujumbe wa Twitter ambapo ameandika kwamba, uamuzi wa Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia wa kuzidisha uzalishaji mafuta, ulikuwa uamuzi wa pupa ambao uliathiriwa na hasira kuhusu msimamo wa serikali ya Moscow.
Wakati huo huo wabunge kadhaa wa chama cha Republican katika bunge la Kongresi nchini Marekani sambamba na kutuma barua kwa Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, wamesisitiza kuwa hatua za Saudia na Russia katika soko la mafuta, zinahatarisha maslahi ya kitaifa ya Marekani. Katika barua hiyo wajumbe hao wa Marekani wametoa onyo didi ya mtu yeyote anayetaka kuvuruga uthabiti wa soko la mafuta duniani.
Katika uwanja huo Kevin McCarthy, kiongozi wa walio wachache katika bunge la wawakilishi nchini Marekani pia ameitaka serikali ya nchi hiyo kukabiliana na ushawishi wa Saudia na Russia katika soko la mafuta duniani.
Awali Dan Sullivan, Seneta wa Republican nchini humo aliionya Saudia kwamba iwapo haitofanya juhudi za kurejesha uthabiti kwenye soko la mafuta, basi atawasilisha mpango wa kuondolewa askari wa Marekani katika nchi hiyo.