Russia: Wapinzani wa JCPOA wanakusudia kudunisha ushirikiano wa Iran na IAEA
Mwakilishi wa kudumu wa Russia katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao mjini Vienna nchini Austria amesema wapinzani wa makubaliano ya nyuklia yaliyosainiwa baina ya Iran na madola makubwa duniani mwaka 2015 wanalenga kudunisha na kudhalilisha muamana na ushirikiano baina ya Tehran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Mikhail Ulyanov amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter jana Jumatatu ambapo ameeleza bayana kuwa: Lengo la JCPOA ni kurejesha imani juu ya malengo ya amani ya miradi ya nyuklia ya Iran. Mapatano hayo yanakidhi wajibu huu. Hakuna dalili ya mkengeuko wa kijeshi iliyoonekana."
Ulyanov ameongeza kuwa, "lengo la wapinzani ni kinyume (na hayo), kudogosha imani na ushirikiano baina ya Tehran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA)."
Hivi karibuni pia, mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Russia alisisitiza kuwa, Marekani haiwezi kulitumia azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kurefusha muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran unaomalizika ndani ya miezi michache ijayo.
Sambamba na kukaribia muda uliowekwa kwa ajili ya kuondolewa vikwazo vya Umoja wa Mataifa vya silaha dhidi ya Iran, ambayo ni sehemu ya azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama, Marekani imezidisha maradufu hatua inazochukua kuzuia mchakato wa kuhitimishwa vikwazo hivyo.
Marufuku iliyokuwa imewekwa ya kutoiuzia Iran silaha kulingana na vifungu vya azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa itaondolewa Oktoba 18, mwaka huu wa 2020, jambo ambalo linaitia kiwewe Marekani.