May 30, 2020 08:14 UTC
  • Trump awatisha waandamanaji wanaolalamikia ukatili Polisi Marekani dhidi ya Wamarekani Weusi

Ukatili usio na kikomo wa Jeshi la Polisi nchini Marekani dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika au Wamarekani weusi ambao unafanyika katika fremu ya sera jumla za ubaguzi wa rangi dhidi ya kaumu hiyo umeibua malalamiko makubwa katika siku za hivi karibuni nchini humo. Malalamiko hayo yameibuka baada ya Mmarekani mweusi kuuawa kinyama siku chache zilizopita mikononi mwa afisa wa polisi mzungu.

Pamoja na hayo, badala ya rais wa Marekani kutafakari namna ya kutatua tatizo hilo, ametoa vitisho dhidi ya waandamanaji.  Mapema Ijumaa, Rais Donald Trump wa Marekani aliandika ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter na kuwataja waandamanaji wanaolalamikia mauaji ya Mmarekani mweusi kuwa ni magenge ya wahuni na wahalifu. Katika ujumbe wake huo, Trump alisema haiwezekani serikali kuwa mtazamaji tu wa mandamano hayo na aliwatishia waandamanaji kwa kusema watapigwa risasi na polisi.  Kufuatia maandishi hayo, Shirika la Mtandao wa Kijamii wa Twitter limesema maandishi hayo ya vitisho ya Trump hayafai na hivyo limemtahadharisha. Shirika la Twitter limesema kuwa ujumbe wa  kwanza wa Trump katika Twitter baada ya maandamano makubwa ya kulaani kuuawa George Floyd mikononi mwa polisi ulikiuka taratibu za mtandao huo wa kijamii na ulihimiza utumiaji mabavu na ukatili. Trump alitumia maneno makali sana dhidi ya waandamanaji waliokuwa na hasira katika mji wa Minneapolis. Katika ujumbe wake wa awali kuhusiana na tukio hilo rais huyo wa Marekani alitumia maneno makali na kudai kuwa: "Hawa wahuni wanavunjia heshima kumbukumbu ya George Floyd na mimi sitaruhusu jambo kama hili liendelee. Trump aliandika: "Nimewasiliana na Gavana  Tim Walz wa jimbo la Minnesota  na nimemfahamisha kuwa atapata uungaji mkono kamili wa Jeshi na Gadi ya Kitaifa Marekani. Pamoja na matatizo yote yanayojiri, tutaweza kudhibiti hali ya mambo. Iwapo uasi na uporaji wa maduka utaanza, waibua fujo watafyatuliwa risasi."

Afisa wa polisi wa Marekani akiwa amemkanyaga Floyd na kumuua 

Katika mauaji mapya ya kibaguzi ya polisi wa Marekani Jumatatu iliyopita afisa mmoja wa polisi mzungu alimuua kwa namna ya kikatili George Floyd (46) Mmarekani mwenye asili ya Afrika kwa kumbana shingo na goti la mguu wake wa kushoto. Floyd alikuwa akipiga kelele kwa kusema: "Umenibana shingo siwezi kupumua," "naomba maji" na "usiniue" hadi alipofariki dunia.  Kufuatia jinai hiyo, wakazi wa mji wa Minneapolis, jimbo la Minnesota wamefanya maandamano makubwa ya kulaani jinai hiyo huku wakitaka wahusika wachukuliwe hatua kali.Polisi wametumia nguvu ziada kukabiliana na waandamanaji waliokuwa wakilalamika kwa amani. Polisi wa kuzima ghasia wametumia gesi ya kutoa machozi, risasi za plastiki na gurunedi dhidi ya wandamanaji Katika maandamano hayo Mmarekani mwingine mweusi ameuawa kwa kupigwa risasi mjini hapo.

Ili kuondoa tuhuma za mielekeo yake ya ubaguzi wa rangi, Trump alituma ujumbe katika Twitter na kudai kuwa amesikitishwa sana na mauaji ya George Floyd mikononi mwa polisi mjini Minneapolis. Hii ni katika hali ambayo katika siku za nyuma, Trump aliunga mkono au kunyamazia kimya ukatili wa polisi wazungu dhidi ya Wamarekani weusi. Hivi sasa Trump anataka kutumia kadhia ya Minneapolis kuonyesha kuwa anasikitishwa na yaliyojiri. Baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kuwa hatua ya Trump kubadili ghafla msimamo wake ni mbinu ya kipropaganda kwa ajili ya kupata kura za Wamarekani wenye asili ya Afrika katika uchaguzi wa rais utakao fanyika Novemba mwaka huu.

Kuongezeka ukatili wa Jeshi la Polisi la Marekani dhidi ya Wamarekani weusi kumepelekea Bunge la Kongresi kuonyesha radiamali. Jerrold Nadler, Mkuu wa Kamati ya Sheria katika bunge la wawakilishi nchini Marekani pamoja na idadi kadhaa ya wabunge wa chama cha upinzani cha Democrat kwenye kamati hiyo wamemtaka William Barr, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Marekani kuchunguza mienendo isiyo ya kisheria ya polisi na asasi zenye mfungamano na idara hiyo. Barua hiyo imetaja majina ya Wamarekani weusi waliouawa kikatili na polisi ya Marekani akiwamo George Floyd aliyeuawa na Minneapolis, Ahmaud Arbery aliyeuawa na afisa wa zamani wa polisi  na Breonna Taylor aliyeuawa huko Kentucky nyumbani kwake kwa kupigwa risasi.

Maandamano mjini Minneapolis 

Barua wa wabunge hao wa Marekani imesema: "Imani ya wananchi kuhusu kutekelezwa sheria kwa uadilifu na bila ya ubaguzi baada ya mauaji tofauti yanayojiri dhidi ya watu wenye asili ya Afrika nchini, imekabiliwa na shaka sana."  

Pamoja na kuwepo ombi hilo lakini ushahidi unaonyesha ubaguzi wa rangi umejikita mizizi katika tasisi na idara za Marekani na hakuna hatua zozote za kivitendo zilizochukuliwa kusitisha utumizi wa mabavu dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika au kuwafanya wawe sawa kijamii na wazungu. Ubaguzi huu uliokita mizizi Marekani umepelekea kuongezeka hasira za raia wasiokuwa wazungu nchini humo na ndio sababu kukashuhudiwa ghasia mjini Minneapolis. Jibu la Serikali ya Kifederali ya Marekani limedhihirika katika vitisho vya Trump ambapo waandamanaji wanaolalmikia ubaguzi wametishiwa kuwa watapigwa risasi iwapo wataendeleza malalamiko yao.

 

Tags