Ujerumani yalikosoa Baraza la Usalama la UN, yasema limepooza na kudumaa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i61906-ujerumani_yalikosoa_baraza_la_usalama_la_un_yasema_limepooza_na_kudumaa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amelikosoa vikali Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akisema limeshindwa kutekeleza majukumu yake.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jun 29, 2020 22:00 UTC
  • Heiko Maas
    Heiko Maas

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amelikosoa vikali Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akisema limeshindwa kutekeleza majukumu yake.

Heiko Maas ameyasema hayo kabla ya Ujerumani kushika usukani wa kuliongoza Baraza la Usalama kwa kipindi cha mwezi mmoja ujao. Amesema Baraza la Usalama limepooza na kudumaa na kuongeza kuwa, linashindwa hata kufikia mwafaka katika masuala na maudhui muhimu kama mgogoro wa Syria na maambukizi ya virusi vya corona kutokana na hitilafu za kimitazamo na mivutano mingi inayotawala baina ya wanachama wake wa kudumu.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Maas amesema kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linashindwa kutimiza matakwa ya walimwengu kuhusiana na maudhui muhimu kama maambukizi ya sasa ya virusi vya corona.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani ameongeza kuwa, kimya cha Baraza la Usalama katika kipindi cha sasa cha kasi kubwa ya maambukizi ya corona ni jambo lisilokubalika kabisa.

Awali jumuiya kadhaa za kimataifa likiwemo shirika la Oxfam zilikuwa zimelituhumu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, limeshindwa kusimamia mapatano ya kusitisha vita na mapigano katika pembe mbalimbali za dunia katika kipindi cha sasa ya maambukizi ya virusi vya corona.