Russia: Marekani inakabiliwa na mzozo mkubwa wa kisiasa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema mivutano na mizozo ya kisiasa ya ndani ya nchi ndiyo sababu kuu iliyoipelekea Marekani iibue madai yasiyo na msingi dhidi ya Moscow.
Sergei Lavrov amesema hayo na kuongeza kuwa, "mzozo wa ndani wa kisiasa ndiyo sababu ya kuibuliwa tuhuma zisizo na mashiko kuhusu eti uhusiano wa Moscow na kundi la wapiganaji wa Taliban nchini Afghanistan."
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia amekosoa vikali madai ya Marekani kuwa Moscow ililipa rushwa kundi la Taliban ili liuwe askari wa Marekani na NATO nchini Afghanistan.
Hivi karibuni, Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo Pentagon ilitoa ripoti ikidai kwamba, serikali ya Russia imeshirikiana na Taliban kwa ajili ya "kuharakisha kuondoka askari wa Marekani" nchini Afghanistan.
Katika ripoti hiyo iliyopewa jina la "Uimarishaji usalama na uthabiti Afghanistan", Pentagon imedai pia kuwa, Moscow inashirikiana na Taliban kuidhoofisha serikali ya Afghanistan.
Hata hivyo madai hayo yamekadhibishwa vikali na Taliban, Russia na hata Rais Donald Trump wa Marekani mwenyewe.