Tishio jipya la Donald Trump dhidi ya Venezuela
(last modified Sun, 12 Jul 2020 12:35:35 GMT )
Jul 12, 2020 12:35 UTC
  • Tishio jipya la Donald Trump dhidi ya Venezuela

Katika hali ambayo siasa za chuki na hasama za Marekani dhidi ya Venezuela hadi sasa zimeshindwa na kugonga mwamba, Rais Donald Trump kwa mara nyingine tena ametoa matamshi ya vitisho kwa kusema: Kuna mambo yatatokea kuhusiana na Venezuela.

Hata hivyo Trump hakuashiria kwa undani mpango na hatua ambazo Washington inapanga kuchukua dhidi ya Venezuela.

Uhusiano na Marekani na Venezuela hususan katika kipindi cha miaka minne iliyopita umezorota na kuharibika mno. Mwenendo huo umeshadidi zaidi baada ya Trump kushika hatamu za uongozini nchini Marekani. Viongozi wa Marekani daima wamekuwa wakizitazama nchi za Amerika ya Latini kama uwanja na ukumbi wao wa kujifaragua na kueneza satwa zao ambapo wameshadidisha mashinikizo yao dhidi ya Venezuela kwa kutumia “Kanuni ya Monroe”.

 Kwa mujibu wa “Kanuni ya Monroe” ambayo ilitangazwa mwanzoni mwa karne ya 19 na Rais wa wakati huo wa Marekani James Monroe, Washington inajitambua kuwa msimamizi na mmiliki wa eneo la Amerika ya Latini na ni kwa sababu hiyo ndio maana daima imekuwa na utendaji wa chuki na hasama na imekuwa ikifanya njama za kuwapindua viongozi na serikali za mrengo wa kushoto katika eneo hilo ambazo zinakwenda kinyume na maslahi ya Washington. Utendaji huo wa Marekani umekuwa kipaumbele cha sera na siasa zake kuhusiana na eneo hilo, utendaji ambao chimbuko lake ni moyo wa kiistikabri na kibeberu wa Marekani.

Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela anayeungwa mkono na Marekani

John Bolton, mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Marekani sambamba na kuashiria “Kanuni ya Monroe” anasema kuwa: Marekani ina haki ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi za Latin Amerika ili iweze kufikia malengo ya Kanuni ya Monroe.

Kuanzia mwaka uliopita wa 2019, Marekani ikiwa na lengo la kuongeza mashinikizo dhidi ya serikali ya mrengo wa kushoto ya Rais Nicolas Maduro ambayo iko dhidi ya ubeberu ilianza kutekeleza vikwazo mbalimbali na vizito dhidi ya Venezuela. Kwa mujibu wa vikwazo hivyo, serikali ya Marekani ilipiga marufuku ununuzi wa mafuta ya Shirika la Taifa la Mafuta la Venezuela. Aidha hata mataifa au mashirika ya kigeni endapo katika mabadilishano yao ya kibiashara ya mafuta yatatumia mfumo wa kibenki wa Marekani yatakabiliwa na faini na vikwazo vya Washington.  Hatua ya Marekani ya kuiwekea Venezuela vikwazo vya kifedha, kibenki na vile vile vikwazo vya dawa na chakula sambamba na njama tofauti za kutekeleza mapinduzi bila kusahau kuwaimarisha wapinzani wa ndani kwa kuwapatia fedha na suhula mbalimbali ni sehemu nyingine ya hatua za Washington dhidi ya Caracas.

Akizungumzia mipango hiyo michafu ya Marekani, Jorge Arreaza, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Venezuela amesema bayana kwamba: Lengo la serikali ya Washington ni kupora vyanzo vya utajiri vya eneo hilo na kuziweka madarakani tawala ambazo zitadhamini maslahi ya Ikulu ya White. Ni kwa muktadha huo, ndio maana nchi za Amerika ya Latini daima zimekuwa zikiandamwa na njama za mapinduzi, hatua za kuteteresha usalama, ugaidi na mzingiro wa kiuchumi, kibiashara na kifedha.

Kilele cha njama za Marekani kilishuhudiwa pale Washington ilipotangaza kinagaubaga kumuunga mkono Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela ambaye Januari mwaka jana alijitangaza kuwa Rais wa nchi hiyo. Hata hivyo licha ya Guaido kupata himaya na uungaji mkono wa kila upande wa Marekani, lakini hadi sasa ameshindwa kuchukua hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Kuendelea kushuhudiwa himaya na uungaji mkono wa wananchi wa Venezuela na jeshi la nchi hiyo kwa serikali ya Rais Nicolas Maduro kumesambaratisha kabisa ndogo za Juan Guaido za kutwaa madaraka ya nchi jambo ambalo hata viongozi wa Marekani wanaonekana kulikiri hadharani.

Kuhusiana na hilo, Donald Trump amenukuliwa akisema wazi wazi kwamba: Sina imani na Juan Guaido. Licha ya Guaido kupata uungaji mkono wa Marekani na madola mengine lakini ameshindwa kufikia malengo yake.

Vitisho vya Marekani dhidi ya Venezuela vinaendelea katika hali ambayo, katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita mikakati miwili ya Washington iliyokuwa na lengo la kuiondoa madarakani serikali ya Maduro imegonga ukuta na kushindwa vibaya. Kusambaratishwa njama za kigaidi dhidi ya Vebnezuela na kutiwa mbaroni mamluki wake na kalikadhila kuweza nchi hiyo kudhamini mahitaji yake ya nishati ya mafuta kutoka Iran na kuwasili meli za mafuta za Iran katika maji ya Venezuela, linahesabiwa kuwa pigo kubwa dhidi ya viongozi wa Washington.

Rais Nicolas Maduro

Samuel Moncada, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Venezuela katika Umoja wa Mataifa anasema: Kuwasili mafuta ya Iran huko Venezuela kwa ajili ya wananchi wa nchi hiyo ilikuwa nukta muhimu sana kwa ajili ya kupigania na kutetea uhuru, mamlaka ya kujitawala na amani.

Hivi sasa kwa mara nyingine tena Rais wa Marekani ametoa matamshi ya vitisho dhidi ya Venezuela kwa sura isiyo ya wazi. Vitisho hivyo vinatolewa katika hali ambayo, viongozi wa Venezuela daima wamekuwa wakieleza utayari wa nchi hiyo wa kusambaratisha njama na tishio lolote lile dhidi ya nchi hiyo na kusisitiza kwamba, sambamba na kulinda mamlaka ya kujitawala na uhuru wake mbele ya matakwa haramu ya Washington, taifa hilo katu halitainamisha kichwa chake na kuonyesha ishara ya utii kwa dola hilo la kibeberu. Inaonekna kuwa viongozi wa Marekani wangali wanafanya hima na njama za kutumia vitisho ili kufunika kushindwa kwao mara kwa mara na taifa la Venezuela.

Tags