Mlipuko mpya wa corona wapiga kengele barani Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i62448-mlipuko_mpya_wa_corona_wapiga_kengele_barani_ulaya
Mlipuko mpya wa virusi vya corona barani Ulaya umepiga kengele ya hatiri kwa watu wa bara hilo huku viongozi wa nchi mbalimbali wakisisitiza udharura wa kuchungwa na kufuata protokali za masuala ya afya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 27, 2020 05:03 UTC
  • Mlipuko mpya wa corona wapiga kengele barani Ulaya

Mlipuko mpya wa virusi vya corona barani Ulaya umepiga kengele ya hatiri kwa watu wa bara hilo huku viongozi wa nchi mbalimbali wakisisitiza udharura wa kuchungwa na kufuata protokali za masuala ya afya.

Msemaji wa Shirika la Afya Dunia (WHO) kanda ya Ulaya amesema kwamba maambukizi ya virusi vya corona barani humo yameongezeka sana katika wiki mbili zilizopita na kuongeza kuwa, mlipuko mpya wa ugonjwa wa COVID-19 katika baadhi ya nchi za Ulaya unatokana na kupuuzwa protokali na sheria za masuala ya afya ya kipindi cha corona.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Ufaransa Jean Castex amewaasa wananchi wa nchi hiyo wasifanye safari katika jimbo la Catalonia la kaskazini mwa Uhispania baada ya serikali ya nchi hiyo kufunga migahawa na klabu za usiku kutokana na ongezeko la maambukizi ya corona. 

Ijumaa iliyopita pia serikali ya Uingereza iliwaamuru raia wote kuvaa barakoa wanapotoka nje kwa ajili ya kununua bidhaa madukani, masokoni na kwa ajili ya shughuli za kibenki.

Nchini Austria pia serikali imewaamuru watu wote kuvaa barakoa wanapotoa nje kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama masokoni, madukani, idara za serikali, kwenye vyombo vya usafiri wa umma, mahospitalini na kadhalika.  

Hatua kama hizo pia zimetangazwa katika nchi nyingine kadhaa za Ulaya.

Bara la Ulaya ndilo linaloongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu walioaga dunia kutokana na virusi vya corona. Hadi sasa zaidi ya watu milioni tatu wameambukizwa virusi vya corona barani humo na zaidi ya nusu yao wako katika nchi za Uingereza, Uhispania, Italia na Russia.