China; Changamoto kubwa zaidi inayoikereketa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i62656-china_changamoto_kubwa_zaidi_inayoikereketa_marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa China amekosoa kwa mara nyingine kuwepo kwa jeshi la Marekani katika Bahari ya China Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 06, 2020 21:53 UTC
  • China; Changamoto kubwa zaidi inayoikereketa Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa China amekosoa kwa mara nyingine kuwepo kwa jeshi la Marekani katika Bahari ya China Kusini.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing, Wang Yi amesema kuhusu kuendelea kuwepo jeshi la Marekani katika Bahari ya China Kusini kwamba, inapasa nchi za eneo hilo ziwe macho na kutoiruhusu Washington iyaharibu na kuyafisidi mafanikio yaliyopatikana ya kuleta amani na ustawi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China amebainisha pia kwamba, Beijing inapinga kwa nguvu zote uanzishaji wa "Vita Vipya Baridi".

Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi

Masuali yanayoulizwa na wengi hivi sasa, ni kwa nini, na licha ya maingiliano mapana ya kiuchumi ziliyonayo, China na Marekani zimekuwa zikivutana na kutunishiana misuli katika nyuga mbalimbali? Kitu gani hasa kinachoisukuma Marekani kushadidisha mivutano baina yake na China? Na kwa nini baadhi ya wataalamu wanayataja makabiliano yanayoendelea kujiri kati ya China na Marekani kuwa ni aina mpya ya Vita Baridi?

Jambo lisilo na shaka ni kuwa, uhusiano wa China na Marekani umeshuhudia mivutano katika kipindi cha karibuni kutokana na sera za uingiliaji mambo za Washington katika eneo linaloizunguka China.

Kwa sasa Washington na Beijing zimejiingiza kwenye mivutano mikali inayozidi kuongezeka baina yao katika nyanja za biashara, uchumi, masuala ya kisiasa, Taiwan, Korea Kaskazini, kadhia zinazohusiana na Asia Magharibi, thamani ya dola, Bahari ya Kusini, Bahari ya Mashariki na vile vile kuhusiana na masuala ya sayansi na teknolojia.

Tab'an viongozi wa China na Marekani kila mmoja ana tafsiri yake kuhusu sababu ya tofauti na mivutano iliyopo baina ya nchi hizo mbili. Viongozi wa Beijing wanasema, uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya China na eneo linaloizunguka ndicho chanzo cha mivutano hiyo. Lakini kwa mtazamo wa viongozi wa Washington, kuzidi kupata nguvu China katika nyuga na sekta mbali mbali ndio sababu ya mivutano iliyozuka katika kipindi cha karibuni baina ya pande hizo mbili.

Kwa maneno mengine ni kuwa, ionavyo Marekani, si masuala ya kisiasa pekee yakiwemo ya Taiwan na Korea Kaskazini, lakini katika hali ya hivi sasa, Washington inaichukulia China kuwa ni mshindani wake hatari katika nyuga za uchumi, sayansi na teknolojia.

Huenda ikawa ni sahihi kusema kuwa, katika miongo michache ya karibuni, hakuna nchi yoyote iliyoweza kuichachafya Marekani kama China na kuifanya iwe na wasiwasi mkubwa kiusalama.

Lisilo na shaka ni kuwa, nguvu na uwezo wa Beijing unaoongezeka kila uchao unawanyima usingizi viongozi wa Washington, mpaka wamefika hadi ya kutoona aibu kutamka hadharani kuwa, China ndiyo tishio kubwa zaidi na changamoto kubwa zaidi kwa Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo amesema kuhusiana na jambo hilo kwamba: "China ndiyo changamoto nambari moja na suala muhimu zaidi katika sera za nje za Marekani."

Si Pompeo peke yake, lakini John Rood, aliyekuwa Naibu Waziri wa Ulinzi wa Marekani, naye pia amesema kuhusu nafasi ya China kwamba: "Leo hii China imekuwa nchi kubwa zaidi yenye uwezo wa kubadilisha njia za maisha za Marekani na nidhamu ya dunia; iwe nidhamu hiyo ni nzuri au mbaya."

Tony Thomas, jenerali mstaafu wa jeshi la Marekani, yeye anakiri kuwa uhusiano baina ya nchi mbili umekuwa tata mno, sambamba na kusisitiza kwamba, Washington haina nia ya kutunishiana misuli kijeshi na China. Jenerali Thomas anasema: "China ndio changamoto kubwa kabisa kiteknolojia kwa Marekani, na katika uga huu hatujawahi kupata changamoto kubwa lakini sasa China imesimama kukabiliana nasi ana kwa ana."

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya kisiasa, tangu China iwe ndilo dola nambari mbili lenye nguvu kubwa zaidi kiuchumi duniani na White House kuhisi kuwa hilo ni jambo hatari kwa Marekani, imejifunga kibwebwe kuzuia na kudhibiti kasi ya nchi hiyo.

Ukweli ni kwamba bila China kufyatua hata risasi moja imeweza kubadilika na kuwa nguvu na changamoto kubwa kwa Marekani, kama yanavyokiri pia mashirika ya intelijensia na viongozi wa nchi hiyo. Lililo wazi ni kuwa, uwezo wa juu wa China katika nyuga tofauti kuanzia za kiuchumi na kijeshi mpaka za sayansi na teknolojia umekuwa ni kengele ya hatari kwa maslahi ya Washington.

Hata hivyo baadhi ya wataalamu wanaamini kuwa mikakati inayotumiwa na Marekani kukabiliana na China na nchi nyinginezo haitaweza kuwa na tija kwa Washington.../