China: Misimamo ya kisiasa iepukwe katika kukabiliana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i62666-china_misimamo_ya_kisiasa_iepukwe_katika_kukabiliana_na_ugaidi
Mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa ametilia mkazo udharura wa kuwekwa kando mienendo ya kindumakuwili na misimamo ya kisiasa katika kupambana na ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 07, 2020 02:32 UTC
  • Zhang Jun
    Zhang Jun

Mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa ametilia mkazo udharura wa kuwekwa kando mienendo ya kindumakuwili na misimamo ya kisiasa katika kupambana na ugaidi.

Zhang Jun jana alikiambia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu ugaidi na uhalifu wa kupanga kwamba, jamii ya kimataifa inalazimika kulinda umoja na mshikamano wake katika kukabiliana na vitisho vinavyosababishwa na ugaidi.

Afisa huyo wa China ametilia mkazo udharura wa kujiepusha na sera za kindumakuwili na misimamo ya kisiasa katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa amezitaka nchi mbalimbali duniani kushikamana na sera za kambi kadhaa na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kukabiliana kwa pamoja na tishio la ugaidi na uhalifu wa kupanga.

Zhang Jun amesema China daima inaunga mkono mtazamo wa kuwepo kambi kadhaa na uadilifu wa kimataifa na kwamba Beijing itaendeleza ushirikiano wake wa kimataifa hususan na nchi zinazostawi kwa ajili ya kukabiliana na ugaidi na uhalifu wa kupanga.