Uturuki, Qatar na Libya kushirikiana kijeshi
Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya imesema imefikiana na Uturuki na Qatar juu ya kutia saini mkataba wa pande tatu wa ushirikiano wa kijeshi na kwamba miongoni mwa nukta muhimu za ushirikiano huo ni kujenga kituo cha kijeshi cha Uturuki katika Bandari ya Misrata nchini Libya.
Nchi hizo tati pia zimeafiki kuwa kutakuwa kukifanyika mkutano kila mwezi katika ngazi ya wakuu wa majeshi ya Libya, Qatar, na Uturuki katika Bandari ya Misrata.
Halikadhalika pande tatu zimeafiki kuwa, Qatar itachangia katika ujenzi na ukarabati wa vituo vyote vya usalama na kijeshi katika mji wa Tripoli ambavyo vimeharibiwa katika vita vya hivi karibuni.
Siku ya Jumatatu ya jana, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Hulusi Akar alifanya mkutano wa pande tatu na mwenzake wa Qatar Khalid bin Mohammad Al Attiyah na Waziri Mkuu wa Libya Fayyez al-Sarraj mjini Tripoli.
Mwezi November, 2019, Ankara na Tripoli zilisaini mapatano ya ushirikiano wa kijeshi na pia katika masua la mipaka ya baharini mashariki mwa Mediterania.
Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, iliyoko karibu na Jenerali Haftar ambayo inapata himaya ya Misri, UAE, Saudi Arabi na baadhi ya nchi za Ulaya, na nyingine ni Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj ambayo inasaidiwa na Uturuki na Qatar. Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ina makao makuu katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.